1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukiukaji wa haki wakati wa vita vya Lebanon

P.Martin2 Desemba 2006

Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu imesema,Israel ilazimishwe kulipa fidia,hasa kwa wale raia waliopata hasara,kwa sababu ya mashambulio ya Israel ya mwezi mmoja,nchini Lebanon.

https://p.dw.com/p/CHL4

Tume hiyo yenye wajumbe watatu imependekeza kuanzishwe mradi wa kimataifa wa fidia,sawa na ule uliolipa mabilioni ya dola kufidia hasara iliyosababishwa na uvamizi wa Irak nchini Kuwait mwaka 1990 hadi 1991.Lakini,tume hiyo imesema,Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva ndio litaachiwa kupitisha uamuzi wo wote ule.

Ripoti iliyotolewa na tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Novemba 21,imeituhumu Israel kuwa imekiuka haki za binadamu katika vita vya Lebanon.Imesema Israel ina hatia ya kutumia nguvu iliyopindukia kiasi na vile vile haikuchagua pa kushambulia,wakati wa vita vya Julai na Agosti.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulio hayo yamesababisha vifo 1,191 nchini Lebanon na nyumba 30,000 ziliteketezwa.Ripoti hiyo pia imesema,Israel nayo ilipata hasara kubwa kutokana na mashambulio ya Hezbollah.Raia 43 waliuawa na nyumba 6,000 ziliharibiwa.

Mjumbe mmoja wa tume hiyo ya uchunguzi,Stelios Perrakis amesema,viwanda vya uvuvi na kilimo nchini Lebanon vimeharibiwa kwa mashambulio ya Israel.Vile vile mafuta yaliomwagika baada ya vituo vya kusafishia mafuta kushambuliwa, yametawanyika na kusambaa hadi Cyprus,Uturuki na Ugiriki.Akaongezea kuwa tume hiyo ya uchunguzi imethibitisha kwamba Israel,inawajibika kimataifa kwa vitendo vyake vya ukiukaji na hasara iliyosababishwa.Alipozungumza na waandishi wa habari,Perrakis alikumbusha kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunda halmashauri iliyosimamia malipo ya Irak,kufidia hasara iliyosababishwa nchini Kuwait.Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilikwenda Lebanon kuchunguza ukweli wa hali,kuambatana na mamlaka ya Baraza la Haki za Binadamu.Israel lakini imepinga uchunguzi huo ikisema ujumbe huo haukufikiria wanamgambo wa Hezbollah waliorusha maroketi 4,000 dhidi ya Israel wakati wa vita vya siku 33.Balozi wa Israel,Itzhak Levanon mjini Geneva alisema,tume hiyo imetoa ripoti isio na usawa.Akaongezea kuwa ripoti ya Umoja wa Mataifa imefanya kosa,kupuuza wajibu wa Lebanon kuzuia ardhi yake kutumiwa kwa vitendo vya kiadui na wajibu wa kuwanyanganya silaha na kuyavunja makundi ya Hezbollah.

Wakati huo huo balozi wa Marekani Warren Tichenor alisema,“Hakuna ripoti inayoweza kuaminika,ikiwa itajaribu kuchunguza habari na kupitisha maamuzi kuhusu mapambano,bila ya kuchunguza vitendo vya pande zote mbili.

Israel ililivamia eneo la kusini la Lebanon baada ya Hezbollah kuwateka nyara wanajeshi wake wawili katika shambulio la mpakani tarehe 12 Julai.