1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Israel wawasili Cairo kwa majadiliano kuhusu Gaza

Hawa Bihoga
25 Agosti 2024

Majadiliano kuhusu usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza yanatazamiwa kuendelea, baada ya ujumbe wa Israel kuwasili nchini Misri leo. Ujumbe huo wa watu 13 umehusisha wawakilishi kutoka serikali ya Israel.

https://p.dw.com/p/4jtpp
Cairo, Misri | Waandamanaji wanaounga mkono Palestina
Baadhi wa waandamanaji mjini Cairo wanaounga mkono PalestinaPicha: MOHAMED ABD EL GHANY/REUTERS

Kundi la Hamas pia limetuma wawakilishi mjini Cairo, wakiongozwa na afisa wa juu Khalil al-Haya. Kama ilivyokuwa kabla, Hamas haitaki kushiriki mazungumzo hayo, lakini inataka kufahamishwa kuhusu maendeleo yake.

Sawa na ilivyokuwa katika duru ya karibuni zaidi nchini Qatar, lengo la mazungumzo ya sasa ni kuziba mianya katika misimamo ya Hamas na Israel na kufikia makubaliano juu ya kusitisha vita. 

Kwa kuwa Hamas na Israel hazijadiliani moja kwa moja, Marekani, Qatar na Misri zinafanya kazi ya upatanishi.

Soma pia:Wajumbe wa Hamas wako Cairo wakati hali ya kibinaadamu ikizidi kuwa mbaya Gaza

Mfalme Tamim bin Hamad Athani, amekwenda Misri kuiwakilisha Qatar, huku mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani, CIA, William Burns, na mratibu wa taifa wa masuala ya Mashariki ya Kati Brett McGurk wakishiriki kwa niaba ya Marerkani. 

Wakuu wa mashirika ya ujasusi wa ndani na nje wa Israel, David Barnea na Ronen Bar pia wamekwenda Cairo.

Mazungumzo kuhusu Gaza yanahusishwa na matumaini ya kuzuwia kutanuka zaidi kwa vita katika Mashariki ya Kati. Israel na Hezbollah, ambayo ni mshirika wa Hamas, zimekabiliana leo, katika mmoja ya mashambulizi makali zaidi katika miezi kadhaa.