1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatambua kufanya mauaji ya kimbari Namibia

28 Mei 2021

Ujerumani kwa mara ya kwanza imetambua kufanya mauaji ya kimbari Namibia wakati wa ukoloni. Imeahidi kuipa Namibia msaada wa kifedha wenye thamani ya euro bilioni moja kusaidia miradi ya kulijenga taifa hilo la Afrika.

https://p.dw.com/p/3u5Pm
Namibia Windhuk | Denkmal zur Erinnerung an den Völkermord an den Herero und Nama
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz

Walowezi wa kikoloni wa Ujerumani waliwaua makumi kwa maelfu ya watu wa asili wa Herero na Wanama kutoka mwaka 1904-1908 - yanayotajwa na wanahistoria kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari ya karne ya 20 na kuharibu uhusiano kati ya Namibia na Ujerumani kwa miaka mingi.

Ingawa Ujerumani imewahi kukubali kwamba ukatili mkubwa ulitokea mikononi mwa mamlaka yake ya kikoloni, kwa muda mrefu imekuwa ikikataa kuilipa Namibia fidia ya moja kwa moja ya kifedha.

Katika taarifa yake, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas kuanzia sasa matukio hayo ya kikatili yatakuwa yakitambuliwa kuwa ni mauaji ya kimbari.

Soma zaidi: Kwa kiwango gani Ujerumani inautambua uovu wa ukoloni wake?

Maas alisifu makubaliano hayo baada ya mazungumzo ya zaidi ya miaka mitano na Namibia juu ya matukio hayo yaliyofanywa na Ujerumani kutoka 1884 hadi 1915.

Ameongeza kwamba Ujerumani, itaiomba Namibia msamaha pamoja na vizazi vya wahanga kwa "ukatili uliofanywa. Na kwamba kama ishara ya kutambua mateso makubwa yaliyowafika wahanga hao, Ujerumani itaunga mkono "ujenzi na maendeleo" ya Namibia kupitia mpango wa kifedha wa euro bilioni 1.1.

Symbolbild Flaggen Deutschland Namibia
Bendera ya Namibia (kushoto) na ya Ujerumani (kulia).Picha: Imago/R. Zöllner

Fedha hizo zitalipwa katika kipindi cha miaka 30, kulingana na duru zilizoshiriki katika makubaliano hayo, na sharti zinufaishe vizazi vya wahanga wa mauaji hayo ya kimbari wanaotoka katika jamii za Herero na Nama.

Maelfu ya Waherero na Wanama waliuliwa 

Namibia ilikuwa ikiitwa Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani wakati wa ukoloni wa Kijerumani kutoka mwaka 1884 hadi 1915, na kisha ikatawaliwa na Afrika Kusini kwa miaka 75 kabla ya kupata uhuru wake mnamo mwaka 1990.

Soma zaidi:Ni lini Ujerumani itaiomba msamaha Namibia juu ya mauaji?

Mnamo mwaka 1904 kulizuka ghasia baada ya watu wa jamii ya Herero waliopokonywa mifugo na ardhi zao kupambana na wanajeshi wa Kijerumani na baadae kuungwa mkono na watu wa jamii ya Nama lakini ujasiri wao huo haukufua dafu mbele ya nguvu ya Kijerumani.

Waherero wapatao 60,000 na karibu Wanama 10,000 waliuawa kati ya mwaka 1904 na 1908. Askari wa kikoloni waliwauwa kwa makundi; wanaume, wanawake, na watoto waliohamishiwa jangwani ambako maelfu walikufa kwa kiu ya maji; wakiwa wameshikiliwa katika kambi yenye mazingira mabaya sana.

Ukatili huo uliofanywa wakati wa ukoloni uliathiri uhusiano kati ya Ujerumani na Namibia kwa miaka mingi.

Vyanzo: afp,rtre