1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasema Hezbollah sio kundi la kigaidi

9 Machi 2019

Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Niels Annen ameliambia jarida la habari la Der Spiegel kuwa vuguvugu hilo la Waislamu wa madhehebu ya Shia linaloungwa mkono na Iran, ni muhimu katika jamii nchini Lebanon

https://p.dw.com/p/3EhW8
Libanon Wahlen
Picha: Reuters/A. Taher

Matamshi hayo yamekuja baada ya Uingereza mwezi uliopta kulipiga marufuku tawi la kisiasa la Hezbollah, ikilutuhumu vuguvugu hilo kwa kuidhoofisha Mashariki ya Kati.

Annen amesema hatua ya Uingereza ni uamuzi wa kitaifa na hauna athari ya moja kwa moja kwa msimamo wa serikali ya Ujerumani wala Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya tayari umeliongeza tawi la kijeshi la Hezbollah kwenye orodha ya makundi ya kigaidi yaliyopigwa marufuku katika mwaka wa 2013. Hezbollah inawakilishwa katika bunge la Lebanon na inashikilia tatu kati ya nyadhifa 30 za uwaziri katika serikali ya Waziri Mkuu Saad al-Hariri inayoungwa mkono na mtaifa ya Magharibi

Tawi la kijeshi la vuguvugu hilo limeimarisha ushawishi wake katika miaka ya karibuni nchini Lebanon na Syria, ambako pamoja na Iran na Urusi linaunga mkono utawala wa Rais wa Syria Bashar al Assad. Nchini Lebabon, linazingatiwa kuwa na nguvu zaidi kuliko jeshi la Lebanon.

Niels Annen
Niels Annen ni mwanasiasa wa SPDPicha: picture-alliance/dpa/G. Wendt

Kiongozi wa Hezbollah atoa ombi la mchango

Mapema Ijumaa, Kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah alisema nchi nyingine huenda zikaufuata mfano wa Uingereza katika wakati ambao Marekani inaimarisha shinikizo la vikwazo dhidi ya kundi hilo.

"Vikwazo na orodha ya ugadi ni mbinu ya kivita dhidi ya vuguvugu letu na lazima tukabiliane nao inavyotakikana” alisema kupitia hotuba ya televisheni, akitoa wito kwa wafuasi wao kuliunga mkono vuguvugu hilo kwa kutoa mchango.

Uwezo wa nguvu za kijeshi wa Hezbollah na umiliki wa aina mbalimbali ya makombora unaipa wasiwasi Israel, na kuongeza uwezekano wa kuanzishwa tena vita baina ya pande hizo mbili

Berlin inaangazia ufumbuzi wa kisiasa

Annen, aliyezungumza na Der Spiegel baada ya ziara nchini Lebanon, alipinga ukosoaji wa Marekani kuwa Ujerumani haifanyi juhudi za kutosha kupambana na ushawishi wa Iran katika kanda hiyo. Alisema sera ya kigeni ya Ujerumani inaendelea kulenga katika kutafuta ufumbuzi wa kisiasa kwa masuala magumu.

Ujerumani na Umoja wa Ulaya zinadhamiria kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya 2015 na Iran, kwa kuweka mfumo mbadala wa ufadhili wa kifedha ili kuruhusu biashara na Iran licha ya vikwazo vya upande mmoja kutoka kwa Marekani.

Lebanona inawahifadhi karibu wakimbizi milioni moja wa Syria, ambapo wengine wameanza kurejea nyumbani wakati vita nchini humo vikielekea kuisha. Mgogoro wa kiutu umefanya kurejea nyumbani kwa njia salama wakimbizi wa Kisyria kuwa suala muhimu kwa Ujerumani.