Ujerumani yamtaka Assad aache maneno matupu
7 Januari 2013Mapigano makali yamezuka katika eneo ambalo ni karibu sana na ukumbi wa sanaa za maigizo mjini Damascus ambao Rais Assad aliutumia kuhutubia umma hapo jana. Mapigano yamefanyika pia katika eneo la karibu na uwanja wa ndege mjini humo.
Kundi moja linalounga mkono wapinzani nchini humo limesema kuwa mizinga vya vikosi vya serikali viliipiga wilaya ya Arqaba ambayo iko umbali wa kilometa tatu tu kutoka ukumbi alioutumia Assad kuhutubia.
Mapigano hayo yalianza tangu jana na kuendelea usiku mzima hadi leo ambapo watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa.
Katika mji wa kaskazini wa Aleppo wakaazi wa eneo hilo walishuhudia pia mashambulizi makali kutoka vikosi vya serikali ambayo pia yanaarifiwa kutokea katika jimbo la kusini la Idlib.
Wakaazi wa mji wa Damascus wameliambia shirika la habari la Reuters hii leo kuwa hotuba ya Assad ilipokelewa kwa shangwe huku milio ya risasi ikisikika katika maeneo ambayo yanakaliwa na wafuasi wake.
Lakini wanasema kuwa hata huko kwa wafuasi wa Assad hakukuwa na dalili ya amani na kwamba waliyatarajia hayo kutokana na kauli za kiongozi huyo za jana zilizolenga tu kuhalalisha mauaji dhidi ya raia na mapigano yanayoendelea.
Shirika la habari la Syria SANA linaarifu kuwa vikosi vya serikali vimefanikiwa kuyadhibiti mashambuizi ya waasi dhidi ya kituo cha mafunzo ya polisi ambapo vimewauwa wapiganaji wa upinzani na kuwajeruhi wengine. Hata hivyo shirika hilo halikutaja idadi ya waasi waliokufa na hata waliojeruhiwa.
Ujerumani yapaza sauti yake
Bado mataifa yanaendelea kumwambia rais Assad kuwa ni lazima asitishe mauwaji. Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa wito kwa kiongozi huyo kuviamuru vikosi vyake vya usalama kusitisha mauwaji badala ya kuendelea kutoa hotuba hewa juu ya utayari wake wa kusitisha mapigano. Westerwelle amziita kauli za Assad katika hotuba yake kuwa ni "tupu".
Westerwelle anasema kuwa mwezi Novemba mwaka jana Rais Assad alikiambia kituo cha televisheni cha Urusi kuwa hataondoka nchini humo kwenda uhamishoni kama ilivyosemekana na kwamba ataishi na kufa ndani ya Syria.
Hivi leo baraza la mawaziri nchini humo linakutana katika kikao maalumu ili kuifanyia kazi mipango ya amani iliyopendekezwa na rais Assad katika hotuba yake.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/Afp
Mhariri:Yusuf Saumu