1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaambulia patupu mashindano ya riadha Budapest

28 Agosti 2023

Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Ujerumani imemaliza mashindano ya Riadha ya Dunia yaliyofanyika huko Budapest, Hungary, mikono mitupu, mwaka mmoja tu kabla mashindano ya Olimpiki huko Paris, Ufaransa.

https://p.dw.com/p/4VetE
Mashindano ya Riadha ya Dunia | Budapest 2023 | Julian Weber
Mrusha mkuki wa Ujerumani Julian WeberPicha: ALINA SMUTKO/REUTERS

Mrusha mkuki Julian Weber ndiye aliyekuwa matumaini ya mwisho ya kweli kwa Ujerumani kushinda angalau medali moja ya kufutia jasho ila Jakub Vadlejch kutoka Jamhuri ya Czech alimtoa nyama mdomoni kwa jaribio lake la mwisho la kurusha mkuki na kumpelekea Weber kumaliza katika nafasi ya nne.

Rais wa shirikisho la riadha Jürgen Kessing hakuyatarajia hayo ila Mkurugenzi wa michezo katika shirikisho hilo Jörg Bügner amekiri kwamba pengo lililopo kati ya Ujerumani na nchi zenye wanariadha mahiri ni kubwa mno na kutahitajika juhudi kubwa ili kulipunguza pengo hilo.

Mashindano ya Riadha ya Dunia | Budapest 2023 | Yemisi Ogunleye
Mwanariadha wa Ujerumani Yemisi OgunlayePicha: Stefan Mayer/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Timu ya Ujerumani kwa sehemu kubwa inamtegemea Malaika Mihambo ambaye safari hii hakuweza kushiriki mashindano hayo kutokana na jeraha ila ni timu inayowakosa wanariadha wengine mahiri kama Noah Lyles wa Marekani aliyeshinda mbio za mita 100 na 200 na Faith Kipyegon wa Kenya aliyeshinda mbio za mita 1500 na 5000.