1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kukipiga na Peru na Ubelgiji

27 Januari 2023

Timu ya kandanda ya Ujerumani inataraji kuwakaribisha Peru na Ubelgiji katika mechi za kirafiki baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia, hii ikiwa ni kulingana na shirikisho la soka la Ujerumani, DFB.

https://p.dw.com/p/4MncV
EURO 2020 Fußball Qualifikation Mannschaft Deutschland
Picha: Markus Gilliar/dpa/picture alliance

Ujerumani itaikaribisha timu ya taifa ya Peru katika mechi ya kirafiki itakayochezwa mjini Mainz Machi 25 na siku chache baadae mjini Cologne ambako itakutana na na Ubelgiji. Kocha Hansi Flick sasa anasubiriwa kutangaza kikosi chake kitakachoingia kwenye michezo hiyo miwili na huenda akakitangaza Machi 17.

"Tuna msisimko mkubwa, kila mmoja anafurahi kucheza tena," amesema Flick.

Ujerumani iliondolewa kwa mara ya pili mfululizo katika hatua ya makundi kwenye michuano ya kombe la dunia iliyofanyika Qatar, baada ya awali kuenguliwa huko Urusi mwaka 2018.

Baada ya kurejea nyumbani, mkurugenzi wa timu hiyo Oliver Bierhoff aliachia ngazi na nafasi yake kuchukuliwa na kocha na mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa, Rudi Völler, wakati DFB ikianza maandalizi kwa ajili ya michuano ya Euro 2024 itakayochezwa nchini Ujerumani.

Soma Zaidi: Ubora soka la Ujerumani wafika ukingoni?

"Tuna matumaini makubwa na michuano hiyo na tunataka kuiimarisha timu yetu inayocheza vizuri na kuonyesha ari na mwamko mkubwa wa kuipigania Ujerumani," alisema Flick. "Kwetu sisi, ni muhimu kwa sasa kujaribu vitu vichache, na ni kutokana na hilo, tutafanya maamuzi magumu na yatakayowashangaza wengi," aliongeza.