1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaUjerumani

Ujerumani kukabiliana na historia ya utawala wake Afrika

15 Juni 2023

Serikali ya Ujerumani inasema inataka kukabiliana na urithi wake wa utawala wa kikoloni barani Afrika. Ila yapo mambo inayoshindwa kuyaangazia, kwanini?

https://p.dw.com/p/4SdrG
Deutschland | Rückgabe der Ngonnso Figur gefordert
Picha: Okach George/DW

Kumbukumbu nzuri na yenye kutia uchungu ya pandashuka za mahusiano ya Ujerumani na Tanzania zinapatikana katika Makumbusho ya Historia katika Mji Mkuu wa Ujerumani, Berlin. Mifupa ya tendaguru mwenye umri wa miaka milioni 150, ndiyo inayotawala makumbusho hayo ya Berlin.

Katika miaka ya 1900, mwanapaleontolojia wa Ujerumani na wasaidizi wake wa Afrika waliifukua mifupa hiyo katika mlima wa Tendaguru katika mkoa wa Lindi. Mifupa hiyo ya tendaguru imewavutia wanafunzi na watalii wa Berlin tangu ilipoanza kuonyeshwa katika makumbusho hayo mwaka 1937 ila ni wachache wanaofahamu historia yake.

Philemon Mtoi ni mwanahistoria wa Tanzania anyeamini kwamba mifupo hii ilifika Ujerumani kinyume cha sheria na anaamini kwamba inastahili kuonyeshwa katika nchi yake ya asili kwani ni mojawapo ya mifupa ya wanyama wa kipekee duniani.

Ujerumani Berlin
Jean-Yves Eboumbou Douala Manga Bell, jamaa wa Rudolf Duala Manga Bell Picha: Tobias Schwarz/AFP

Katika siku za hivi karibuni, Ujerumani imejaribu kukabiliana na suala hili la urithi wake wa kikoloni. Waziri wa mambo ya nje Annalena Baerbock alisafiri kuelekea Nigeria Desemba mwaka uliopita ili kurudisha shaba za Beninnchini Nigeria. Shaba hizo ziliibwa na wanajeshi wa Uingereza katika nchi iliyokuwa wa kifalme ya Benin ambayo kwa sasa iko Nigeria na kisha zikauzwa katika makumbusho ya Ujerumani.

Karibu mafuvu 200 ya vichwa yatarudishwa Tanzania, pamoja na mengine 900 nchini Rwanda ambayo pamoja na Burundi na sehemu ndogo za Msumbiji kaskazini ziliunda utawala wa Ujerumani Afrika Mashariki.

Mwanasiasa wa Ujerumani Sevim Dagdelen, kutoka chama cha upinzani cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto, ana maoni ya kwamba Ujerumani inastahili kufanya juhudi zaidi za kuchunguza urithi iliyouacha Afrika Mashariki kati ya mwaka 1885 na 1918.

Dagdelen na wanasiasa wengine wa mrengo wa kushoto hivi majuzi waliwasilisha maswali katika bunge la Ujerumani na mojawapo ya maswali makuu ya Dagdelen ambalo bado halijajibiwa ilikuwa ni iwapo hatua ya majeshi ya ukoloni ya Ujerumani ya kuwaangamiza wapiganaji wa Maji Maji kusini mashariki mwa iliyokuwa Tanganyika, inaweza kutajwa kama mauaji ya halaiki kwa matazamo wa dunia ya leo.Baerbock kurudisha mwenyewe kazi za sanaa Nigeria

Kati ya mwaka 1905 na 1907 Wajerumani waliwaangamiza wapiganaji wa Maji Maji kwa njia za kinyama. Inakadiriwa kwamba kati ya watu laki mbili na laki tatu walifariki dunia, huku vyanzo vya vifo hivyo vikiwa kuuwawa kwenye mapigano, kufichwa kwa mifugo na vyakula na magonjwa na utapiamlo.

Baadhi ya wanazuoni wamepata ushahidi mkubwa kuunga mkono madai ya mauaji ya halaiki katika vitendo vilivyofanywa na Ujerumani nchini Tanzania.

Shaba za Benin
Baadhi ya kazi za sanaa zilizoporwa Afrika na UjerumaniPicha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Katika jawabu lake bungeni, serikali ya Ujerumani ilikiri kwamba inafahamu jinsi mauaji hayo ya Maji Maji yalivyofanywa ila ililikwepa swali la mauaji ya halaiki na badala yake ikasema, inalijua jukumu lake la kimaadili na kisiasa kutokana na mazungumzo ya kuaminiana iliyofanya na serikali ya Tanzania.

Baerbock kurudisha mwenyewe kazi za sanaa NigeriaMwanahistoria Jürgen Zimmerer anaamini kwamba serikali ya Ujerumani inalikwepa swala hilo kwa sababu ina wasiwasi kuhusiana na yatakayofuata baadae. Anasema serikali ya Ujerumani ilifikiri kwamba inaweza kulifutilia mbali suala la mauaji ya Namibia ambayo ilikiri kwamba yalikuwa mauaji ya halaiki na ikalazimika kulipa fidia kwa familia ingawa kiwango ilichokipendekeza bado hakijakubaliwa Namibia.

Na sasa wanasiasa hao wa mrengo wa kushoto Ujerumani pia wameibua suala la fidia ila jawabu la serikali ya Ujerumani ni kwamba serikali ya Tanzania bado haijawasilisha malalamiko rasmi ya kudai fidia.

Lakini mwanahistoria wa Tanzania, Philemon Mtoi anasema ni makosa kuisubiri serikali ya Tanzania kuwasilisha hitaji kama hilo, kwani Ujerumani inastahili kuonyesha ishara ya wazi ya kutaka maridhiano kwani isipofanya hivyo sasa, basi mahusiano yatavurugika kwa miaka mingi ijayo.