Ujerumani kuendeleza marufuku dhidi ya matukio makubwa
27 Agosti 2020Kansela Merkel anatarajiwa kufanya mkutano kwa njia ya vidio na viongozi wa majimbo 16 ya Ujerumani kujadili hatua za nchi nzima za kukabiliana na maambukizi zaidi ya virusi vya corona, ikiwemo pia suala la kuwapima watu wanaorejea kutoka nje ya Ujerumani. Kwa hivi sasa suala la upimaji bure virusi vya corona ni kwa watu wanaowasili Ujerumani wakitokea nje ya nchi na pia ni lazima katika maeneo ya mipaka kwa watu wanaorejea kutoka kwenye nchi zilizoanishwa kuwa katika hatari kubwa.
Katika mapendekezo yatakayojadiliwa na viongozi hao, matamasha makubwa ya muziki, mashabiki kuruhusiwa kuingia kwenye viwanja vya michezo vyote hivyo huenda vikasubiri hadi mwishoni mwa mwezi Desemba ingawa kunaweza kuwepo na upekee kwa majimbo yaliyo na maambukizi kidogo. Uamuzi huo utakuwa pigo kwa klabu za Ujerumani ambazo zilikuwa na matumaini ya kukutana na mashabiki wao tena viwanjani katika msimu mpya. Mipango mingine ni kupunguza idadi ya watu wanaoweza kukutana katika mikusanyiko midogo ya hadi watu 25.
Pia viongozi hao walitarajiwa kujadili utekelezaji wa sheria kali juu ya uvaaji barakoa na faini ya kiwango cha chini cha euro 50 ikiwa mtu atashindwa kutekeleza masharti hayo. Hadi sasa kila jimbo hapa Ujerumani limekuwa na faini zake zinazotofautiana kuanzia euro 40 mjini Hamburg hadi euro 250 huko Bavaria.
Siku ya Jumatano mji wa Berlin ulipiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa juma kupinga sheria zilizowekwa za kupambana na virusi vya corona. Mamlaka za Berlin zimesema sababu ya kuzuia maandamano ya Jumamosi ni wasiwasi kwamba waandamanaji hawatozingatia kanuni za usafi kama vile kukaa umbali wa mita 1.5.
Waandaaji wa maandamano wanasema watu takribani 20,000 walipanga kuhudhuria, wakiongeza uamuzi wa kuyapiga marufuku umechochewa kisiasa na watapinga suala hilo mahakamani. Waziri wa mambo ya ndani wa Berlin Andreas Geisel, akiongeza kuwa "kwa kuzingatia ongezeko la visa vya corona mjini berlin na Ujerumani, mikutano kama hiyo ya maelfu ya watu ambapo tunadhani kwamba kanuni za kupambana na virusi hivyo zitakiukuwa, ni hatari kubwa. ndio maana mamlaka zimechukua uamuzi kama huo na naunga mkono." Soma Ujerumani inakabiliwa na wimbi la pili la virusi vya Corona
Mara ya mwisho Kansela Merkel alikutana na wakuu wa majimbo mwezi Juni pale walipotangaza kulegeza masharti ya kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo ambayo yalionekana kupungua. Hadi sasa, Ujerumani imeripoti kesi mpya 1,507 na kufanya idadi jumla kufikia 237,936 kwa mujibu wa taasisi ya udhibiti magonjwa ya Robert Koch na idadi vifo imefikia 9,285.