1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaadhimisha miaka 34 ya muungano

Angela Mdungu
3 Oktoba 2024

Ujerumani inaadhimisha miaka 34 ya kuungana kwa pande mbili za nchi hiyo. Shamrashamra za maadhimisho hayo zinafanyika mjini Schwerin huku kukitarajiwa maandamano ya Muungano unaopinga vita kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/4lMuE
Maadhimisho ya siku ya Muungano wa Ujerumani
Shamrashamra za maadhimisho ya Muungano wa Ujerumani zilizoanza 02.10.2024 jioni mjini SchwerinPicha: Jens Büttner/dpa/picture alliance

Maadhimisho ya muungano wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na Magharibi hufanyika katika miji tofauti ya Ujerumani, na mwaka huu yako katika mji mkuu wa jimbo la Mecklenburg -Vorpommern linalopatikana katika upande wa kaskazini mashariki mwa taifa hilo. Hii ni mara ya tatu kwa jimbo hilo kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya muungano wa Ujerumani.

Kansela Olaf Scholz na Rais Frank Walter Steinmeier wanahudhuria hafla hiyo yenye wageni waalikwa 450. Mbali na viongozi hao wa ngazi ya juu ya kitaifa watakaopata nafasi ya kuhutubia, Mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern, Manuela Schwesig anatarajiwa pia kuzungumza.

Majimbo yote, Bunge, Baraza la juu la Bunge sambamba na taasisi mbalimbali zinawakilishwa kwenye maadhimisho hayo wakati ikiwa ni siku rasmi ya mapumziko kote Ujerumani.

Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi ziliungana mwaka 1990 baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, mwishoni mwa zama za vita baridi.

Muungano wa kupiga vita wapanga kuandamana

Katika hatua nyingine, muungano wa kupinga vita nchini Ujerumani unaojulikana kama  "Never Again War" utafanya maandamano. Kwa mwaka huu maandamano hayo yamejikita katika kupinga mipango ya kuwepo kwa makombora ya Marekani katika ardhi ya Ujerumani. Mpango huo ulitangazwa na Kansela Scholz kuwa utaanza kutekelezwa mwaka 2026.

Waandamanaji wanapanga pia kuonesha upinzani wao dhidi ya vita vinavyoendelea kushika kasi Ukraine na Mashariki ya kati. Hatua ya Ujerumani kupeleka silaha Ukraine na Israel ni suala jingine lililo katika orodha ya masuala yanayopingwa katika maandamano hayo.

Maandamano yaliyofanyika Belin kupinga vita Gaza Mei 18,2024
Maandamano ya kuiunga mkono Palestina yaliyofanyika Berlin Mei 18, 2024Picha: RALF HIRSCHBERGER / AFP

Miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuzungumza katika maandamano ya mwisho yatakayofanyika mjini Berlin ni pamoja na Mwanasiasa Sarah Wagenknecht anayefuata siasa za mrengo wa kushoto. Mwanasiasa wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha SPD Ralf Stegner pamoja na Gesine Lötzsch wa Die Linke nao pia watatoa hotuba zao.

Muungano huo unatoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kusitisha haraka mivutano kati ya Urusi na Ukraine, na katika vita vinavyoendelea Gaza.

Chama cha raia wa Ukraine waishio Ujerumani kilishatoa taarifa ya kufanya maandamano ya kuyazima maandamano ya Muungano wa Kupinga vita yaliyopewa jina la, "Amani yenu ni hukumu ya kifo kwetu".