1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Ujerumani: Hali ya Sudan inapaswa kupewa uzito

Angela Mdungu
28 Novemba 2024

Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze, amesema dunia inahitaji kuitilia maanani hali ya kuvunja moyo inayoendelea nchini Sudan. Ameyasema baada ya kurejea kutoka kwenye ziara yake nchini humo.

https://p.dw.com/p/4nWpj
Wakimbizi wa Sudan waliokimbilia Chad
Kambi ya wakimbizi wa Sudan mjini Adre, ChadPicha: Sam Mednick/AP

Katika mahojiano yake na DW Waziri huyo wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani amezungumzia kuhusu kiwango kikubwa  cha janga la kiutu alichokishuhudia Sudan na kile mataifa tajiri yanachoweza kukifanya ili kuisaidia nchi hiyo inayokabiliwa na vita.

Amesema wakimbizi wanaokimbilia Chad kutoka Sudan wanapitia hali ngumu wanapokuwa safarini. Akizungumzia hali iliyo katika mpaka wa nchi hizo mbili, Bi Schulze  amesema kuwa Chad ni moja ya mataifa masikini zaidi duniani lakini imefungua milango kuwapokea wakimbizi kutoka Sudan wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Soma zaidi: Wanamgambo wa RSF wa Sudan watuhumiwa kuwaua watu 40

Itakumbukwa kuwa, zaidi ya wakimbizi 700,000 wa Sudan wamelazimika kukimbilia Chad. Waziri Schulze ameisifu nchi hiyo kwa kuonesha mshikamano na wakimbizi hao na kuwa dunia inapaswa kuziona na kuzitambua juhudi hizo.

Hivi karibuni, wakati Schulze alipoitembelea Chad Ujerumani ilitangaza mpango wa kuipa baada ya kupokea wakimbizi wa Sudan. Aliutembelea mji mkuu Ndjamena na kuzungumza na serikali na wawakilishi wa mashirika ya kiraia kuhusu hali hiyo na mahitaji yao. 

Mataifa yanapaswa kuzishinikiza pande hasimu kusitisha vita

Alipoulizwa ikiwa mataifa tajiri kama Ujerumani yanaupuuza mzozo huo na kujikita katika vita Migogoro ya Mashariki ya Kati na Ukraine, Waziri Schulze amejibu kwamba ulimwengu una haja ya kuzidi kutazama zaidi kinachoendelea Sudan na kuongeza shinikizo kwa pande hasimu za mgogoro huo.

Svenja Schulze katika mahojiano na DW TV
Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani Svenja SchulzePicha: DW

Taifa la Sudan, lilitumbukia katika vita Aprili 2023 kutokana na ugomvi wa madaraka kati ya kundi la wapiganaji wa RSF linaloongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Daglo na jeshi rasmi la serikali chini ya Jenerali Abdel Fattah Al  Burhan.

Soma zaidi: UN: Washirika wanaopeana silaha Sudan walaumiwa

Pande hizo mbili za mzozo zimekuwa zikishutumiwa kwa kufanya vitendo vya uhalifu wa kivita vikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya makazi ya watu, masoko na hospitali.

Hadi sasa maelfu ya watu wameuwawa na zaidi ya milioni 11 wamelazimika kuyahama makazi yao kulingana na Umoja wa Mataifa. Takwimu za shirika hilo zinaonesha pia kuwa, ndani ya Sudan, mtu mmoja kati ya watano hana makazi kutokana na vita vinavyoendelea sasa au vilivyopita.

Umoja wa Mataifa unasema, pande zote za mzozo nchini humo zimekuwa zikitumia njaa kama silaha katika vita hivyo. Mamlaka zinadaiwa kwamba zimekuwa zikikwamisha juhudi za kufikisha misaada nchini humo kwa kuweka vizingiti vya urasimu wakati wapiganaji wa RSF wakiwatisha na kuwavamia wafanya kazi wa mashirika ya misaada.