1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza, Ufaransa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Omicron

Angela Mdungu
14 Desemba 2021

Waziri mkuu wa Uingereza amewataka wafanyakazi zaidi wa kujitolea wajitokeze katika vituo vya kutolea chanjo ili kukabiliana na aina mpya ya virusi vya corona, Omicron

https://p.dw.com/p/44Fjb
Neue COVID-19-Variante Omicron
Picha: Pavlo Gonchar/Zumapress/picture alliance

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amewaomba maelfu ya wafanyakazi wa kujitolea kuchukua nafasi katika vituo vipya vya chanjo kwenye maeneo ya maduka na viwanja vya michezo wakati serikali ikiongeza kasi ya programu yake ya kupambana na aina mpya ya virusi vya corona, Omicron.

Hatua hiyo ni baada ya waziri mkuu Johnson kuweka lengo jipya la chanjo kwa watu wazima hadi kufikia mwishoni mwa huu wakati wizara ya afya nchini humo ikiripoti kuwa virusi hivyo vipya vya Omicron sasa vinaambukiza karibu watu 200,000 kila siku. Mapema leo, waziri wa afya wa Uingereza Dominic Raab alisema Uingereza hadi sasa ina wagonjwa 10 waliolazwa hospitali kutokana na virusi vya Omicron.

Wakati hayo yakiendelea, Johnson anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa chama cha wahafidhina kuhusu kura itakayopigwa baadaye leo bungeni ili kuamua juu ya kuwekwa kwa hatua mpya zinazolenga kukabiliana na janga la virusi vya corona. 

Hatua hizo zinajumuisha kuwataka watu wafanyie kazi nyumbani, kuvaa barakoa maeneo ya wazi na kutumia vibali maalumu vya COVID 19 vinavyomruhusu mtu kuingia katika baadhi ya kumbi.

Ufaransa kudhibiti mipaka zaidi

Nchini Ufaransa, serikali imesema leo huenda ikaweka udhibiti mkali zaidi katika mipaka yake  ili kujilinda dhidi ya virusi vya Omicron ambavyo vimeshaambukizwa kwa watu wengi kwenye taifa jirani la Uingereza. Ufaransa kwa sasa inawataka watu wanaowasili kutoka nje ya mipaka yake kuwa na kipimo kilichofanywa ndani ya saa 48 kinachothibitisha kuwa mtu hana maambukizi, hata kama mtu huyo tayari alishapata chanjo.

Großbritannien London | Ansprache Boris Johnson zu Omicron
Waziri mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Tim Hammond/Avalon/Photoshot/picture alliance

Msemaji wa serikali ya Ufaransa Gabriel Attal amesema maafisa wake wakati wote wanaangalia namna ya kuimarisha zaidi sheria katika maeneo ya mipaka. Ameongeza kuwa maamuzi juu ya matumizi ya sheria kali zaidi za udhibiti wa maambukizi yatafanyika siku chache zijazo.

Nako Marekani, jeshi la anga nchini humo limewafuta kazi maafisa 27 kwa kukataa kupata chanjo dhidi ya ugonja wa virusi vya corona. Jeshi la anga la Marekani liliwapa wanajeshi wake muda hadi Novemba 2 wawe wameshapata chanjo na maelfu kati yao wamekuwa wakikataa au kukwepa kufanya hivyo kwa kutoa sababu mbalimali. Msemaji wa jeshi hilo Ann Stefanek alisema jana Jumatatu kuwa maafisa waliofutwa kazi ni wa kwanza kufukuzwa kwa masuala yanayohusiana na chanjo.