1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Tutafuata sera yetu kuwapeleka wahamiaji Rwanda

15 Juni 2022

Baada ya mahakama ya Ulaya kuhusu Haki za Binadamu kusitisha safari ya ndege ya wahamiaji kuelekea Kigali Rwanda, Uingereza imeapa kufuata sera yao ya uhamiaji ili kufanikisha mpango huo ambao umekosolewa pakubwa.

https://p.dw.com/p/4CjAR
UK | Abschiebeflug nach Ruanda
Picha: Finnbarr Webster/Getty Images

Uingereza imeapa Jumatano kwamba itafuata sera yake yenye utata ya kuwasafirisha wahamiaji ambao waliyakataa maombi yao ya hifadhi hadi nchini Rwanda, baada ya Mahakama ya Ulaya inayoshughulikia Haki za Binadamu kutoa uamuzi wa kisheria uliofuta mnamo dakika za mwisho safari ya ndege ya kwanza iliyopangwa kuwapeleka wahamiaji hao. Uamuzi huo ni pigo la aibu kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson. 

Idadi ya wahamiaji waliopaswa kusafirishwa usiku wa kuamkia leo kutoka London hadi Rwanda, ilikuwa imeshuka kutoka 130 hadi 7 pekee, na mwishowe ikawa hakuna aliyesalia kufuatia agizo la mahakama ya Ulaya kuhusu Haki za Binadamu (ECHR).

Pigo na fedheha kwa Boris Johnson

Kufutwa kwa safari hiyo ni pigo la aibu kwa serikali ya kihafidhina yake waziri mkuu Boris Johnson, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Liz Truss, kusisitiza kwamba ni sharti ndege hiyo iliyopangwa kwenda Kigali ingesafiri wala haijalishi ikiwa na abiria wangapi.

Mpango wa Uingereza kutaka kuwaondoa wahamiaji waliokataa maombi yao ya hifadhi hadi Rwanda imekosolewa pakubwa na Umoja wa Mataifa, wanaharakati na kuzusha maandamano.
Mpango wa Uingereza kutaka kuwaondoa wahamiaji waliokataa maombi yao ya hifadhi hadi Rwanda imekosolewa pakubwa na Umoja wa Mataifa, wanaharakati na kuzusha maandamano.Picha: Niklas Halle'n/AFP/ Getty Images

Shirika la kutetea haki za binadamu kwa jina Care4Calais limesema agizo la ECHR linaweza kuzingatiwa kuwalinda wahamiaji wengine wote wanaotarajiwa kupelekwa Rwanda.

Uingereza imesitisha safari ya kwanza ya waomba hifadhi kwenda Rwanda

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema dhamira yao ni kuhakikisha wameweka mambo bayana hivi kwamba kila mtu anaweza kujionea kuwa hatua yao ni ya haki, kati ya uhamiaji wa kisheria kwa taifa hilo kwa njia salama na kisheria. Kwamba wanaunga mkono na wanalinda kwa sababu wanaelewa manufaa yake. Na waweze kutofautisha hilo na uhamiaji kinyume cha sheria kwa kuvuka bahari kwa njia hatari, jambo wanalotaka kukomesha.

Denmark yazungumza na Rwanda kuhusu upokezi wa wahamiaji

"Ujumbe wangu leo ni kwamba hatutazuiwa au kufedheheshwa kwa njia yoyote na baadhi ya wakosoaji dhidi ya sera yetu, tutasonga mbele kuufanikisha mpango wetu," amesema Johnson

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel amesema amesikitishwa kwamba mapingamizi ya kisheria na madai ya dakika za mwisho yalisababisha safari ya ndege kukatizwa. Hata hivyo, amesisitiza kwamba mpango huo ambao umekosolewa pakubwa utaendelea mbele.

Mahakama ya Haki ya Ulaya ilitoa agizo la kuzuia safari hiyo kama hatua ya kuzuia raia wa Iraq ambaye huenda angeteswa.
Mahakama ya Haki ya Ulaya ilitoa agizo la kuzuia safari hiyo kama hatua ya kuzuia raia wa Iraq ambaye huenda angeteswa.Picha: Niklas Halle'n/AFP/ Getty Images

Kwa nini mahakama ya Haki ya Ulaya ilitoa agizo hilo?

Mahakama ya ECHR ilitoa agizo la kusitisha safari hiyo kama hatua ya kuzuia kusafirishwa kwa raia mmoja wa Iraq aliyekuwa miongoni mwa waliopaswa kusafirishwa, kwa kuwa huenda angeteswa, lakini pia maombi yake ya hifadhi hayakuwa yameshughulikiwa kikamilifu.

Mahakama hiyo iliyoko Strasbourg imesema safari hiyo isubiri hadi kesi za kubaini uhalali wa kisheria wa sera ya Uingereza inayoruhusu usafirishaji huo, iamuliwe na mahakama za Uingereza mwezi Julai.

Patel aliutaja uamuzi wa ECHR kuwa wa kushangaza na akasisitiza wengi walioondolewa kwenye ndege hiyo watasafirishwa katika ndege nyingine.

Rwanda na Uingereza watia mkataba kuhusu uhamiaji

Kwa upande mwingine, Rwanda imesema bado imejitolea kuwapokea wahamiaji wanaoomba hifadhi, kulingana na makubaliano yao ya mwezi Aprili. Makubaliano hayo yamekosolewa pakubwa na Umoja wa Mataifa, mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na viongozi wa kidini.

Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba matukio ya hivi karibuni kusitisha usafirishwaji wa wahamiaji hao, haiizuii nchi yake. Ameongeza kuwa Rwanda iko tayari kuwapokea wahamiaji punde watakapowasili na itawapa usalama na nafasi mbalimbali nchini humo.

 (AFPERTRE)