1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi wa kwanza

14 Juni 2022

Serikali ya Uingereza inatarajiwa kutuma leo nchini Rwanda ndege ya kwanza iliyowabeba waomba hifadhi waliokataliwa nchini Uingereza. Kumekuwa na upinzani na ukosoaji mkubwa kuhusu sera hiyo ya Uingereza

https://p.dw.com/p/4CfXo
Ruanda Kigali | Britische Innenministerin Priti Patel unterzeichnet Abkommen zur Flüchtlingspolitik mit Außenminister Vincent Birutaare
Rwanda na Uingereza zilifikia makubaliano ya waomba hifadhi wanaokataliwaPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Ndege ya kukodishwa inatarajiwa kuondoka mojawapo ya viwanja vya ndege vya London leo usiku na kutua kesho mjini Kigali. Hii ni baada ya majaji wa Uingereza kupinga jana kesi ya rufaa dhidi ya ya hatua hiyo ya kufukuzwa.

Soma pia: Uingereza kuwapeleka Rwanda wanaotafuta hifadhi

Waziri wa mambo ya Kigeni wa Uingereza Liz Truss ameiambia televisheni ya Sky News leo kuwa hawezi kusema hasa ni watu wangapi watakaokuwa kwenye ndege hiyo. "Siwezi kusema gharama ya safari hizo za ndege. Lakini tunachopaswa kuzingatia ni gharama ya uhamiaji haramu. Gharama kwa Uingereza. Gharama kwa watu na familia zao zinazoteseka kutokana na vitendo vya wanaowasafirisha haramu wa watu hawa. Ndicho tunachotaka kushughulikia kwa kushirikiana na Rwanda."

Walalamikaji walihoji kuwa uamuzi kuhusu sera ungepaswa kusubiri hadi kikao kamili cha kusikilizwa mahakamani kuhusu uhalali wa sera hiyo mwezi ujao. 

London | Protest in London
Kumekuwa na maandamano ya kupinga sera ya UingerezaPicha: Niklas HALLE'N/AFP

Wahamiaji 31 wanatarajiwa kupelekwa Rwanda lakini mmoja wa walalamikaji, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali la Care4Calais, limesema kuwa tiketi za watu 23 kati yao sasa zimefutwa. Shirika la Care4Calais linasema wanaotarajiwa kufukuzwa Uingereza ni pamoja na raia wa Albania, Iraq, Iran na Syria.

Mjini Geneva, mkuu wa shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa Filippo Grandi ameikemea sera ya Uingereza akisema yote ni mbaya na kuongeza kuwa nchi hiyo haipaswi kuuhamisha wajibu wake kwa nchi nyingine.

Viongozi wa Kanisa la England, akiwemo Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby, wameongeza sauti zao za uokosoaji wa sera hiyo wakisema inaliaibisha taifa hilo.

Serikali ya Uingereza inasisitiza kuwa sera hiyo inahitajika ili kuzuia mmiminiko wa wahamiaji wanaohatarisha maisha yao kuvuka bahari kutokea Ufaransa.

Chini ya makubaliano na Kigali ya kiasi cha pauni milioni 120 sawa na dola milioni 148, yeyote anayewasili Uingereza kinyume cha sharia atapewa tiketi ya safari ya kwenda bila kurudi kwa ajili ya kushughulikiwa nyaraka zake na kupewa makazi Rwanda. Uingereza inasema waomba hifadhi wenye nyaraka halali wanapaswa kuridhia kuishi Ufaransa. Kinyume na linavyosema UNHCR, Rwanda inasisitiza kuwa ni mahali salama na yenye uwezo wa kuwakaribisha maelfu ya waomba hifadhi Uingereza.

afp, reuters