1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza hatimaye yakamilisha kuondoka Umoja wa Ulaya

1 Januari 2021

Hatimaye Uingereza imetamatisha kabisa uhusiano wake wa nusu karne na Umoja wa Ulaya kwa kujiondoa kutoka kwenye soko moja la Umoja huo na pia kwenye umoja wa forodha.

https://p.dw.com/p/3nQMN
UK London Big Ben 23h nachts
Picha: Tim Ireland/Photoshot/picture alliance

Uingereza sasa itafanya mambo yake kivyake, miaka minne baada ya kura yake iliyoishtua Ulaya ya kutaka kuondoka kwenye Umoja huo, Brexit.

Brexit ilitimia mara tu ilipogonga saa tano usiku kwa saa za Uingerezana saa sita usiku kwa nchi nyengine za Ulaya zilizokuwa zinaadhimisha mwaka mpya wa 2021. Waziri Mkuu Boris Johnson aliyeongoza kampeni ya nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya, amesema hiki ni kipindi kizuri na akaendelea na usemi wake kwamba Uingereza itakuwa "Uingereza ya Dunia" ambayo haitotikiswa na sheria zinazotungwa katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

"Tuna uhuru wetu mikononi mwetu na juu yetu kuutumia vyema uhuru huu," alisema Johnson.

Ukaguzi wa forodha unarudi baada ya miongo kadhaa

Kisheria Uingereza iliondoka kutoka kwenye Umoja wa Ulaya Januari 31 mwaka 2020 ila imekuwa katika kipindi cha mpito wakati wa mazungumzo ya kusaka makubaliano ya kibiashara na umoja huo ambayo yalipatikana mkesha wa Krismasi.

Großbritannien London | Boris Johnson unterzeichnet Brexit-Handelsabkommen
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akitia saini makubaliano ya kibiashara na Umoja wa UlayaPicha: Leon Neal/Getty Images

Na kwasasa kwa kuwa kipindi hicho cha mpito kimeshakwisha, sheria za Umoja wa Ulaya hazitumiki tena kwa Uingereza. Matokeo ya kwanza ya mchakato huo kukamilika ni kikomo cha usafiri huru wa watu milioni 500 kati ya Uingereza na nchi 27 za Umoja wa Ulaya.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo kadhaa, ukaguzi wa forodha unarudi na licha ya makubaliano ya biashara huria yanayotoa nafasi kwa UIngereza kuendelea kufanya biashara na karibu wateja 450 wa Umoja wa Ulaya, kunatarajiwa milolongo mirefu na kutatizwa kwa huduma kutokana na stakabadhi zaidi zitakazohitajika.

Huko Calais, Ufaransa, maafisa wa Ufaransa walianza kutekeleza sheria hizo mpya saa sita usiku juu ya alama ambapo walianza kwa kulikagua trela moja lililokuwa linatokea Romania na lililokuwa limebeba barua.

Uingereza ni nguvu kubwa ya kifedha na kidiplomasia

Uingereza ndiyo mwanachama wa kwanza kuuhama Umoja wa Ulaya uliobuniwa kuleta umoja baada ya mabaya yaliyoshuhudiwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Kura ya maoni ya mwaka 2016 ilileta mivutano mikali baina ya waliokuwa wanataka kubakia Umoja wa Ulaya na waliokuwa wanataka kuondoka na kusababisha miaka kadhaa ya kulemazwa kwa siasa nchini humo kabla Johnson kuchukua uongozi mwaka jana na kuapa kwamba ataifanya Uingereza iwe nchi yenye uvumbuzi wa kisayansi na ushirikiano na nchi mbalimbali.

Belgien Brüssel | Unterzeichnung Brexit Abkommen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Johanna Geron/REUTERS

Uingereza ni nchi yenye uwezo mkubwa wa kifedha na kidiplomasia na pia ni mwanachama mwenye nguvu kubwa katika muungano wa kujihami wa NATO na fauka ya hayo ni nchi iliyo na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia katika nchi saba zilizostawi kiuchumi duniani G7.

Umoja wa Ulaya kwa sasa umpoteza watu milioni 66 na uchumi wa trilioni 2.85 na kuna majuto kwamba Uingereza ilitaka kujiondoa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Uingereza itasalia kuwa "rafiki yetu" lakini akadai kwamba Brexit ni matunda ya mchakato uliokuwa na "hadaa na ahadi za uongo."