1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yafunga tena shughuli zake kutokana na COVID-19

14 Oktoba 2020

Wakati bara la Ulaya likiendelea kupambana na kile kiitwacho "wimbi la pili" la maambukizo ya virusi vya corona, Uholanzi imeamuwa kurejea tena kwenye kuzifunga shughuli za kawaida za kimaisha kwa angalau wiki nne.

https://p.dw.com/p/3jv1z
Niederlande Coronavirus | Krankenschwester in Amsterdam
Picha: Hollandse Hoogte/Imago Images

Idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa maradhi hayo ya COVID-19 nchini Ujerumani imepanda kwa 5,132  siku ya Jumatano, na hivyo kuifanya idadi jumla ya waliokwishaambukizwa hadi sasa kufikia 334, 585 kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch, inayohusika na udhibiti wa maradhi ya maambukizo.

Watu waliopoteza maisha ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita ni 40 na kwa hivyo sasa Ujerumani imeshapoteza watu 9,677. Hii ni sawa na ongezeko la watu 1,000 walioambukizwa na vifo mara mbili zaidi ya hali ilivyokuwa siku ya Jumanne.

Katika kukabiliana na ongezeko hilo, Kansela Angela Merkel anatazamiwa kukutana na mawaziri wakuu wote wa majimbo 16 ya Ujerumani kujadiliana hatua mpya za kudhibiti mripuko huu wa virusi vya corona.

Berlin Kanzlerin Merkel | PK zu Videokonferenz mit Bürgermeistern großer Städte
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Axel Schmidt/AFP

Kansela Merkel alielezea ongezeko hili kote barani Ulaya kwamba ni jambo linalotisha na akawatolea wito watu kuchukuwa tahadhari, kufuata kanuni za kujilinda, kuweka masafa baina yao, kuvaa barakowa na wafanye kila wawezalo kupambana na virusi wakati huo huo wakiendelea na shughuli zao za kuzalisha mali.

Hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesema nchi yake inarejea kwenye ufungaji wa baadhi ya shughuli za kawaida za maisha kuanzia Jumatano, ambapo mabaa, mikahawa na uuzaji wa pombe vimepigwa marufuku, huku maduka ya rejareja yamewekewa muda maalum wa kufunguliwa, na mikusanyiko ya zaidi ya watu wanne ikizuiliwa kabisa.

Vile vile serikali ameamuru uvaaji wa barakowa za vitambaa kwa watu wote wanaonzia umri wa miaka 13 kwenda juu, huku mikutano yote ya ndani ikitakiwa isizidi watu 30. Hata hivyo, skuli pamoja na usafiri wa umma vitaendelea kuwa wazi. Waziri Mkuu Rutte amesema sheria maalum itapitishwa kufanya uvaaji barakowa kuwa jambo la lazima.

Nchini Italia, Waziri Mkuu Giuseppe Conte alisaini dikrii ambayo inaamuru hatua mpya za kuzuwia mikusanyiko ya watu kwenye maeneo ya wazi, mikahawa, michezo na hata skuli. Conte alisema hatua hizo zinachukuliwa ili kuzuwia kufungwa kwa shughuli zote kwa nchi nzima. Uamuzi huu unafuatia kupanda ghafla wa maambukizo, ambapo mwishoni mwa wiki Italia ilisajili watu 6,000 walioambukizwa ndani ya kipindi cha masaa 24.

Italien I Giuseppe Conte zum italienischen Corona-Hilfspaket
Waziri mkuu wa Italia Giuseppe ContePicha: picture-alliance/Xinhua News Agency/A. Lingria

Uingereza nayo imetangaza kile inachokiita mfumo wa pande tatu, ambapo maeneo yenye maambukizo mengi yatalazimika kuchukuwa hatua za haraka kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona kwenye maeneo mengine. Kuanzia leo Jumatano, mji wa Liverpool, ambao uko kwenye nafasi ya juu kabisa kwa maambukizo unaanza hatua za kufunga mabaa na mikusanyiko angalau kwa mwezi mmoja kutoka sasa.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Keir Starmer, amesema ni wazi kuwa serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson imeshindwa kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19.