1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania, Sweden na Uingereza zamtambua Guaido

4 Februari 2019

Shirika la mataifa ya Amerika ya Kusini na Canada linajadili namna ya kuendeleza shinikizo dhidi ya rais wa Venezuela Nicolas Maduro kumtaka kuitisha uchaguzi mpya wakati kukiongezeka na miito ya kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/3CfJY
Spanien Pedro Sanchez
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Comas

Shirika la mataifa ya Amerika ya Kusini na Canada hii leo litajadili namna ya kuendeleza shinikizo dhidi ya rais wa Venezuela Nicolas Maduro kumtaka kuitisha uchaguzi mpya katika wakati ambapo anakabiliwa na ongezeko la miito ya kumtaka kujiuzulu. Maduro hata hivyo anaendelea kuikaidi miito hiyo. 

Wakati mataifa hayo yakikutana, serikali ya Uhispania kupitia waziri wake mkuu wa Pedro Sanchez imetangaza kumtambua Juan Guaido aliyejitangaza kuwa rais wa mpito, baada ya rais Maduro kukaidi mwito wa mataifa ya Ulaya wa kuitisha uchaguzi wa mapema. 

Waziri mkuu Sanchez ametangaza hatua hiyo muda mfupi uliopita mbele ya waandishi wa habari. Uingereza na Sweden nazo zimetangaza kumtambua Guaido kama rais wa mpito wa nchi hiyo.

Mataifa 7 ya Ulaya yalikuwa yamempa Maduro hadi Jumapili ya jana kuwa siku ya mwisho ya kuitisha uchaguzi, vinginevyo wamtambue Guaido. Hata hivyo, rais Maduro ameupuuza muda huyo. 

Venezuela Krise | Präsident Nicolas Maduro in Caracas
Rais Nicolas Maduro anakabiliwa na shinikizo kubwa nchini mwakePicha: Reuters/Miraflores Palace

Maduro amesema kwenye mahojiano yaliyorushwa jana na kituo cha televisheni cha Uhispania Antena 3 kwamba hatakubaliana na masharti ya muda kutoka kwa mtu yoyote, akisisitiza hataitisha uchaguzi wa mapema. Alinukuliwa akisema "Hatutakubali masharti kutoka kwa yoyote. Ni kama vile nikiuambia Umoja wa Ulaya, ninawapa siku saba za kuitambua Jamhuri ya Catalonia, na kama hamtaki tutawachukulia hatua. Hapana, siasa za kimataifa haziwezi kuzingatia masharti. Hayo yalikuwa enzi za Kifalme na ukoloni."

Amesema, uchaguzi wa rais utafanyika mwaka 2024. Maduro ambaye ameendelea kuungwa mkono na jeshi amesema Guaido anaandaa mapinduzi dhidi yake, chini ya maagizo ya Marekani. Hata hivyo anaunga mkono mpango wa mataifa hayo ya Umoja wa Ulaya na Amerika ya Kusini kufanya mazungumzo Alhamisi ijayo ya kusuluhisha mzozo wa Venezuela.

Ofisi ya waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau imesema mkutano wa Ottawa pia utajadili namna ya kuwasaidia raia wa Venezuela, ikiwa ni pamoja na misaada ya dharura ya kiutu. Trudeau alizungumza na Guaido kwa njia ya simu jana, na  walijadili umuhimu wa jumuiya ya kimataifa, hivyo kutuma ujumbe wa wazi kuhusu uhalali wa utawala wa Maduro.

Venezuela Caracas Juan Guaido
Tayari Guaido ameanza kuitambuliwa na mataifa washirika wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa/sincepto/R. Hernandez

Vyanzo mbalimbali vimesema mataifa hayo 14 wanachama wa Azimio la Lima, yameonekana kujiandaa, ingawa yatajizuia kuiwekea vikwazo zaidi serikali ya Maduro wakati yatakapokutana Ottawa, mji mkuu wa Canada. Mataifa 11 miongoni mwake yanamuunga mkono Juan Guaido, kiongozi wa upinzani aliyetangaza kuwa rais wa mpito.

Guaido anajaribu kumshinikiza Maduro kuachia mamlaka, ili kuunda serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi mpya wa urais. Tayari amelitaka jeshi kuruhusu misaada ya kiutu kuingia nchini humo, kutokana na mzozo mkubwa wa kiuchumi unaolikabili taifa hilo.

Aidha, kiongozi huyo wa upinzani aliyejitangaza rais alitarajiwa kutangaza tarehe ya kuwasili kwa misaada ya kiutu kutoka Marekani, hatua ambayo Maduro anasema itatumika kama njia kwa Marekani kujiingiza kijeshi nchini humo. Guaido, ameitisha maandamano mapya Februari 12, kuongeza shinikizo la kuruhusu misaada hiyo ya kiutu kuingia Venezuela.

Marekani pia inataka Maduro aachie ngazi. Jana, rais Donald Trump alinukuliwa akisema kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS kwamba wanaweza kuiingilia kijeshi Venezuela.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel