1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhasama kati ya Tembo na wakulima kupatiwa ufumbuzi nchini Zambia

Epiphania Buzizi7 Septemba 2005

Wakulima wadogo wadogo katika bonde la mto Zambezi Kusini mwa Zambia, wanalima zao la pilipili kama silaha ya kuzia uharibifu unaofanywa na tembo wanaoharibu mazao mashambani

https://p.dw.com/p/CHeo
Tembo wanalaumiwa kufanya uharibifu wa mazao Kusini mwa Afrika.
Tembo wanalaumiwa kufanya uharibifu wa mazao Kusini mwa Afrika.Picha: AP

Zao la pilipili ambalo linatumiwa na watu wengi kama kiungo, sasa itatumiwa kuondoa uhasama uliokuwepo kati ya wakulima na wanyama waharibifu.

Mkurugenzi wa mradi wa kuendeleza Tembo nchini Zambia, Nina Gibson,amesem kwamba pilipili itatumiwa katika kampeni hiyo kwa sababu tembo hawapendi harufu ya pilipili.

Njia hiyo pia ni rahisi sana kutumia kwani haina gharama yoyote ikilinganishwa na mbinu nyingine za kupambana na uharibifu wa mazao unaofanywa na tembo mashambani.

Maafisa wa hifadhi ya wanyama wanasema kwamba mradi wa kilimo cha pilipili unawasaidia wakulima kupata mazao ya biashara na wakati huo huo kupambana na wanyama waharibifu.

Utafiti huo wa kilimo cha pili pili kama kinga ya kuzuia wanyama waharibifu, kwanza ulianzia kaskazini mwa Zimbabwe n abaada yae kutumika nchini Kenya,Sri Lanka; Laos na Thailand.

Wakulima wanasaga pilipili na kuichanganya na mafuta ya injini zilizochakaa. Mchanganyiko wa vitu hivyo hupakwa kwenye nyaya za nyua zinazozungushiwa mashamba, na hivyo kulinda mazao mashambani.

Njia nyingine inayotumika ni kuchanganya unga wa pilipili na samadi au uchafu unaotokana na wanyama. Mchanganyiko huo huchomwa moto usiku na kutoa moshi mzito ambao huwafukuza tembo.

Mbinu hizi hutumiwa na wakulima wadogo wadogo nchini Zambia ambao hawana uwezo wa kutumia nyua za umeme kutokana na gharama yake kuwa kubwa.

Wakulima wapatao 80 wanajumuika katika mradi huo wa kilimo cha pilipili katika bonde la mto Zambezi na wanachangia sana kilimo cha zao hilo linalopendwa na walinzi wa mazingira.

Sio nchini Zambia pekee ambako kuna tatizo la ongezeko la tembo wanaoharibu mazao mashambani.

Katika nchi za Kenya na Namibia, pia kumeripotiwa ongezeko la wanyama hao wanaokabiliana na wakulima katika maisha yao ya kila siku ya shughuli za kilimo.

Tembo wanaweza kuharibu mashamba katika kijiji kizima na kusababiha athari kubwa kwa mkulima wa kawaida ambaye anategemea kilimo.

Katika nchi hizo wakulima wanawasha moto mkubwa au kupiga ngoma kama njia ya kuwafukuza tembo wanaoharibu mazao mashambani.

Nako nchini Botswana tatizo la tembo limekuwa kubwa na hata wakati mingine wanyama hao huvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Namibia, amabako huangamiza mazao na wakati mwingine kuwararua watoto.

Hata hivyo kazi hiyo ya ulinzi usiku ina hatari zake kwa afya ya wakulima hao ambao huumwa na mbu na kuugua malaria.Mwezi uliopita, serikali ya Kenya ilianzisha operesheni kubwa ya kuwafukuza tembo wapatao 400 kutoka eneo la mwambao wa bahari ya Hindi kunakopatikana makundi mengi ya tembo.

Kampeni hiyo imeendeshwa kwa lengo la kulinda mazingira na kupunguza mzozo uliokuwepo kati ya tembo na wakulima wa maeneo jirani na mbuga za wanyama.

Mzozo kati ya wanadamu na wanyama pori umekithiri na kuchukua sura mpya barani Afrika. Hayo yamebainishwa na Bwana Graeme Petterson wa Kituo cha kimataifa cha kuhidhadhi wanyama ambacho kina makao yake makuu nchini Marekani.

Afisa huyo amesema kuwa anaamini kuwa ikiwa tatizo hilo halitapatiwa ufumbuzi,wakulima watachukua hatua ambazo zitakuwa na athari dhidi yao na hata kwa wanyama.

Umoja wa hifadhi za wanyama Duniani ulisema mwezi June kwamba idadi ya tembo inamidi kuongezeka katika maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika ripoti yake umoja wa hifadhi za awanyama Duniani umebainisha kuwa idadi ya tembo katika kanda hizo mbili za bara la Afrika imeongezeka kutoka tembo 283,000 hadi kufikia 355,000 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2002. Kiwango cha ongezeko hilo ni asilimia 4.5 kwa mwaka.

Lakini pia ongezeko la watu linaendelea kwa kasi kubwa katika mataifa yanayoendelea, na kusababisha mgogoro kati ya wanadamu na wanyama wakubwa wa pori.

Maafisa wa mradi wa kuendeleza kilimo cha pilipili katika bonde la mto Zambezi, wanasema kwamba wakulima wengi wamehamia katika eneo hilo la bonde miaka 20 iliyopita, wakitafuta mashamba kutokana na ukosefu wa ardhi katika maeneo mengine ya nchi yao.