"Uhalifu wa kivita watendeka Syria" - Human Rights Watch
2 Mei 2012Shirika la Human Rights Watch linasema kwamba vikosi vya serikali ya Syria viliwaua kiasi ya raia 95 kati ya mwishoni mwa mwezi Machi na mwanzoni mwa mwezi Aprili na kuzichoma na kuziharibu nyumba za wakaazi wa jimbo la Idlib, katika wakati ambapo mjumbe wa kimataifa, Kofi Annan, akitafuta makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katika ripoti yake iliyochapishwa leo (Jumatano, 02.05.2012) na kupewa jina la "Waliuunguza Moyo Wangu", shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani, limeorodhesha matukio kadhaa ya mauaji, mateso, kamatakamata ovyo na uharibifu wa mali za raia, ambayo linasema yanafikia kiwango cha kuitwa uhalifu wa kivita.
Msaidizi Mkurugenzi wa Mipango na Dharura wa shirika hilo, Anna Neistat, amesema kwamba kila mahala walipokwenda walishuhudia nyumba, gari na maduka yaliyochomwa moto na kuharibiwa, na walipokea taarifa za watu ambao ndugu zake waliuawa.
"Ni kama kwamba vikosi vya serikali ya Syria vilikuwa vikipatiza kutumia kila dakika waliyokuwanayo kusababisha madhara kabla ya kuanza kwa muda wa kusitisha mapigano." Amesema Nestat.
Kisingizio cha kupambana na magaidi
Ikitumia sababu ya kupambana na magaidi wenye silaha, serikali ya Syria imekuwa ikiishambulia miji na vijiji vilivyo ngome za upinzani dhidi yake, ingawa mara kadhaa nyumba za watu wa kawaida ndizo zinazoangukiwa na makombora.
"Sikuwa na magaidi wowote ndani, lakini nyumba yangu imevunjwa kabisa." Amesema mwanamke mmoja kwenye jimbo la Idlib.
Katika ripoti hiyo, shirika la Human Rights Watch limelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa timu yake ya waangalizi inayopelekwa nchini Syria iwe na kitengo maalum cha haki za binaadamu ambacho kinaweza kuchunguza na kuwahoji waathirika kwa uhuru juu ya uvunjwaji wa haki za binaadamu uliofanywa dhidi yao.
Timu hiyo ya waangalizi imepewa jukumu la kuangalia namna usitishwaji wa mapigano unavyoendelea, jambo ambalo ni kipengele muhimu kwenye mpango wa amani wenye vipengele sita uliopendekezwa na Kofi Annan kumaliza miezi 13 ya umwagwaji damu nchini Syria.
Pande zote zavunja makubaliano
Hata hivyo, kuna dalili chache za kuthibitisha usitishwaji wa mapigano kuliko zile zinazoonesha kuendelea kwake, kutoka pande zote mbili. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na Operesheni za Amani, Hervé Ladsous, amesema kwamba "uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unatokea pande zote mbili."
Mapema leo, Shirika la Habari la Syria liliripoti kwamba bomu lililotegwa kando ya barabara lilimuua mwanajeshi mmoja na kuwajeruhi wengine watatu katika jimbo la Hama.
Katika mashambulizi mengine, waasi wamekivamia kikosi cha wanajeshi kwenye jimbo la Allepo na kuwauwa wanajeshi 15. Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lililo na makao yake nchini Uingereza, limesema katika mashambulizi hayo ya asubuhi ya leo waasi wawili waliuawa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman