1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhaba wa chakula kulikumba jimbo la Isiolo nchini Kenya ?

Michael Kwena24 Oktoba 2022

Idara ya elimu jimboni humo,imeeleza kuwa,wanafunzi wengi wamelazimika kusalia nyumbani kwani hawawezi kustahimili makali ya njaa wakiwa shuleni.

https://p.dw.com/p/4IcG5
Kenia Marsabit Pastoralismus
Picha: DW/Michael Kwena

Huko Kenya kumeripotiwa visa vya wanafunzi kadhaa kuzirai katika jimbo la Isiolo nchini kenya, wakiwa shuleni kutokana na  kile kinachoaminika ni kuzidiwa na makali ya njaa.

Visa hivyo vimeripotiwa katika maeneo ya Ngeremara,Oldonyiro na Kina ambapo wanafunzi kadhaa wamekuwa wakizirai kutokana na makali ya njaa katika kaunti ya Isiolo. Mkurugenzi wa elimu katika kaunti hiyo James Nyaga amesema kwamba,makali ya njaa yamelemaza juhudi za masomo katika baadhi ya shule jimboni humo wakati huu.

''Maajuzi tumekuwa na visa viwili''

Kulingana naye,baadhi ya walimu wamehamishwa katika shule zingine kufuatia hatua ya wazazi kuwaondoa watoto wao shuleni wakati hali ya ukame ikizidi kuwa mbaya eneo hilo.

"Tumekuwa na visa vya wanafunzi kuzirai wakiwa kwenye gwaride na hata wakati wakicheza.Maajuzi tumekuwa na visa viwili kule Ngaremara na kule Oldonyiro kulikuwa na shule tatu ambapo wanafunzi walizirai wakati wa mchana. Tuna shule moja ambayo imefungwa katika Kijiji cha Yamicha na walimu wakapelekwa katika shule zingine” alisema Nyaga.

Wizara ya elimu nchini imekuwa ikiendesha mpango wa kuwapa chakula wanafunzi shuleni katika majimbo tofauti tofauti kama sehemu ya kuwawezesha wanafunzi kusalia shuleni na kuendeleza masomo yao bila vikwazo.

Nusu ya wakaazi wa Isiolo wakumbwa na njaa

Umoja wa mataifa umeasaidia  kutoka huduma ya chakula kwenye maeneo yalioathirika
Umoja wa mataifa umeasaidia kutoka huduma ya chakula kwenye maeneo yalioathirikaPicha: WFP/Marcus Prior

Hata hivyo,kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha wazazi jimboni Isiolo Ismael Galma,baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakificha chakula wanachopokea shuleni kuwapelekea jamaa zao nyumbani ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa.

"Mimi nafahamu kuwa,baadhi ya Watoto hubeba chakula wanachopokea shuleni na kuwapelekea wazazi wao nyumbani.Kwa hivyo,chakula cha shule kinasaidia sana…”

Takwimu kutoka mamlaka ya kukabiliana na majanga NDMA jimboni Isiolo,inaonyesha kuwa,nusu ya wakaazi jimboni humo wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa.

Watu wanaoishi na ulemavu aidha,wamo katika orodha ya makundi maalum ya watu wanaohitaji msaada wa chakula wakati huu kama anavyoeleza mwenyekiti wa watu wanaoishi na ulemavu jimboni Isiolo Abdi Wako.
"Baa la njaa limezidi na tunaomba watu wanaoishi na ulemavu pia wape vyakula.''

Ahadi za misaada ya chakula

Kaunti ya Isiolo ni miongoni mwa kaunti nyingine ishirini na tatu ambazo ziko katika hitaji kubwa la msaada wa vyakula wakati serikali ya kitaifa ikiendeleza mpango wa kusambaza vyakula kwa kaunti zinazokabiliwa na hali mbaya ya ukame.

Jana jumapili,naibu wa rais Rigathi Gachagua,alitangaza kwamba,serikali itaanza kusambaza msaada wa chakula leo jumatatu katika majimbo ya kitui,Machakos na makueni baada ya majimbo hayo kuripoti kuhitaji msaada wa dharura wa vyakula.

Hofu ya binadamu kuanza kufariki kutokana na makali ya njaa inawapa wasiwasi mkubwa viongozi kutoka majimbo yaliyoathirika na hali mbaya ya ukame.