Ugiriki: Wahamiaji wahofia majira ya baridi kwenye kambi
28 Septemba 2018Hata wale waliomo kwenye orodha ya kuhamishwa kupelekwa bara baada ya mashirika yasiyo ya kiserikali kufichua hali duni katika kambi hizo wanaomba na kujenga matumaini kwamba safari yao iwe kabla ya mvua za msimu hazijaanza na kuigeuza kambi yao kuwa dimbwi la matope.
Mkimbizi mmoja mwenye umri wa miaka 53 Jamal ambaye anaishi kwenye kambi ya Moria katika kisiwa cha Lesbos anauliza kwa nini Wagiriki hawafanyi chochote wakipata pesa nyingi kuwatunza wakimbizi hao. Kambi hiyo ndio kubwa zaidi nchini Ugiriki. Swali lake linasisitiza hali ya kuchanganyikiwa kwa wakimbizi wengine wengi waliokwama katika kambi hiyo huku serikali ikiwa imeshindwa kutoa hata huduma muhimu zaidi kwa watu hao.
Jamal, raia wa Somalia, alikuja nchini Ugiriki wiki tatu zilizopita pamoja na binti yake mwenye umri wa miaka 21, ambaye ni kipofu na anasumbuliwa na aina nadra na mbaya ya maumivu ya kichwa. Dalili zake hufanana kama vile mtu anapotaka kushikwa na kiharusi, kwa mfano, udhaifu wa misuli na kupooza kwa muda upande mmoja wa mwili wake.
Jamal na binti yake wanaweza kuwa ni wachache wenye bahati, kati ya wakimbizi elfu mbili, watakaofaidika na hatua ya kuhamishiwa bara hapo tarehe 8 mwezi ujao. Mapema mwezi huu, shirika la huduma za Madaktari wasiojali mipaka (MSF) liliripoti matukio mengi ya majaribio ya kutaka kujiua au kujidhuru miongoni mwa wakimbizi waliokwama katika kambi hiyo, ikiwa ni pamoja na watoto .
Wafanyakazi katika kambi hiyo walikuwa tayari wametishia kufanya mgomo kupinga kile ambacho hata serikali ya ugiriki ilikubali kuwa ni hali ngumu kutokana na msongamano wa watu walio kwenye kambi hiyo. Lakini licha ya kufikiwa mkataba mnamo mwaka 2016 kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, wahamiaji wanaendelea kumiminika.
Visiwa vya Lesbos na Samos, ambavyo vina kambi kubwa za wakimbizi, na vipo nchini Ugiriki, japo kuwa vipo nje kidogo ya pwani ya Uturuki, upande wa mashariki wa bahari ya Aegean.Kambi hizo zikabiliana na wahamiaji zaidi ya 20,000 huku wahamiaji 8,000 wakiwa kwenye kambi ya Moria ambayo imejengwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu 3,000 pekee.
Hali katika kambi hiyo inazidisha mambo kuwa mabaya kwa watu ambao tayari wanasumbuliwa na msongo wa mawazo kutokana na yale yaliyowakuta na kuwasababishia kuyakimbia makazi yao. Madaktari wasiojali mipaka pia wameelezea juu ya mapungufu makubwa katika kuwalinda watoto. Thuluthi moja ya watoto kwenye kambi hizo wanatoka Afghanistan na Syria.
Katika kujitetea, Ugiriki inaelezea kwamba wimbi la wahamiaji wapya wanaoendelea kuingia nchini humo na kushindwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia makubaliano ya kugawana wahamiaji ndio chanzo kikubwa cha mateso ya wahamiaji hao.
Mwandishi:Zainsab Aziz/AFPE
Mhariri: Gakuba, Daniel