1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki kusaidiwa?

Abdu Said Mtullya28 Aprili 2010

Viongozi muhimu wakutana mjini Berlin kujadili njia za kuisaidia Ugiriki.

https://p.dw.com/p/N8zA
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa Dominique Strauss-KahnPicha: picture-alliance/dpa

Masoko ya hisa leo yamepanda barani Ulaya kutokana na matumaini kwamba pande muhimu zitasimama pamoja katika kutafuta suluhisho la mgogoro wa Ugiriki kwa kuipatia nchi hiyo fedha ili kuiwezesha kulipa madeni yake.

Kwa mujibu wa habari nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na shirika la fedha la kimataifa IMF zinakusudia kutenga hadi Euro Bilioni 120 kwa ajili ya kuisaidia Ugiriki katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Mashirika ya habari yamemnukulu mbunge wa Ujerumani wa chama cha kijani Jürgen Trittin aliemkariri mkurugenzi wa shirika la IMF Dominique Strauss Kahn akisema Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na shirika lake unakusudia kutenga kiasi hicho cha fedha.

Katika juhudi za kutafuta suluhisho la haraka, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani leo, mjini Berlin, amekutana na mwenyekiti wa benki kuu ya Ulaya Jean-Claude Trichet na mkurugenzi wa shirika la fedha la kimataifa Domique Strauss- Kahn.

Baada ya mkutano huo mkurugenzi wa IMF alisema kuwa pande zinazohusika zitakabiliwa na hali ngumu lakini ameeleza kuwa ana uhakika kwamba suluhisho linaweza kupatikana.Lakini amesema serikali ya Ugiriki katika upande wake inapaswa kuchukua hatua ndefu zaidi.

Iwapo shirika la fedha la kimataifa IMF litatoa fedha kuisaidia Ugiriki na iwapo nchi hiyo itachukua hatua zinazohitajika ,mkurugenzi huyo ameeleza kuwa amepata uhakika kutoka kwa waziri wa fedha wa Ugiriki alieyekutana naye mjini Washington hivi karibuni.Lakini amesema pana haja ya kurejesha imani duniani.

Hatahivyo habari zinasema Ugiriki inapinga baadhi ya masharti.

Hapo awali taasisi inayotathmini uwezo wa nchi wa kupata mikopo Standard and Poors, ilisema dhamana za Ugiriki hazina thamani tena. Ugiriki imefilisika.Mkuregenzi wa shirika la IMF ameitaka Ujerumani ichukue hatua za haraka.ili kuiokoa Ugiriki.Hatahivyo Ujerumani imesisitiza kwamba Ugiriki kuchukua hatua kadhaa kwanza.

Wakati huo huo msemaji wa wizara ya fedha ya Ujerumani Jeanette Schwamberger amearifu kuwa sheria ya kuiruhusu Ujerumani kutoa mchango wake wa fedha katika kuisaidia Ugiriki inaweza kupitishwa kwenye matawi yote mawili ya bunge mnamo muda wa wiki moja ikiwa Ugiriki itakamilisha haraka, mazungumzo yake na Shirika la fedha la kimataifa na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/APE/DPA/ZA.

Mhariri/Abdul-Rahman