1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yawarudisha waasi wa zamani wa DRC kwao

Lugeba Emmanuel (Mhariri: Sekione Kitojo)26 Februari 2019

Uganda imewarudisha kwa hiari waasi wa zamani 57 wa DRC nchini mwao kufuatia mpango unaotekelezwa na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3E7pV
Waasi wa M23 wa DRC wakiwa na silaha (Picha hii ya maktaba ilipigwa 30.11.2012)
Waasi wa M23 wa DRC wakiwa na silaha (Picha hii ya maktaba ilipigwa 30.11.2012)Picha: Imago/Kyodo News

Watu 57 waliokuwa wapiganaji wa kundi la M23 waliokimbilia Uganda wamerudishwa kwa hiari yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hii ni chini ya mpango wa amani,usalama na ushirikiano unaotekelezwa na Umoja Mataifa ukihusisha Umoja wa Afrika na wengine.

Hao ni baadhi ya waliokuwa wapiganaji wa kundi la M23 wakiimba kuonyesha ari na utayari wao kurudi nyumbani Jamhuri ya Kidemokasia ya Congo baada ya kuishi Uganda kwa muda wa miaka mitano. Kundi la wapiganaji 57 pamoja na jamaa zao 10 walisaini mkataba wa kukubali kurudi kwa hiari. 

Waasi wa M23 wakitembea eneo la Ziwa Kivu (Picha ya maktaba)
Waasi wa M23 wakitembea eneo la Ziwa Kivu (Picha ya maktaba)Picha: Getty Images/AFP/P. Moore

Hatua hii imetekelezwa kwa mujibu wa mpango wa amani, usalama na ushirikiano eneo la maziwa makuu ambapo waliokuwa waasi na wapiganaji ikiwemo wale wa FDLR au Interahamwe wa Rwanda nao wanatarajiwa kufanya hivyo. Mchakato wa utekelezaji wa mpango huo ulianza mwaka 2013 katika majadiliano Addis Ababa na kisha baadaye Congo Brazaville ukihusisha Umoja wa Afrika,Jumuiya ya ushirikiano wa kibishara ya SADC, shirika la kimataifa la maziwa makuu ICGLR na serikali za kanda.

Akiwapokea waliokuwa wapiganaji wa M23 balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jean Pierre Massala amesifu mpango huo akiahidi kuwa watu hao watapokelewa na kusaidiwa kuendelea na maisha ya kawaida mara tu watakapofika nchini kwao.

Ndege ya umoja mataifa ndiyo imewasafirisha watu hao kutoka uwanja wa zamani wa Entebbe. Lubega Emmanuel DW Kampala