1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yawarejesha polisi wa Kongo waliokimbia mapigano

16 Agosti 2024

Uganda imewarejesha polisi 100 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokimbia mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo, serikali ya Uganda amesema.

https://p.dw.com/p/4jZPn
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kibumba 2022 | M23
Waasi wa M23 wamekuwa wakifanya mashambulizi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusababisha maelfu kuyakimbia makazi yaoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Taarifa yake imesema baada ya kuthibitisha vitambulisho vya uraia, maafisa hao wa polisi waliruhusiwa kuingia Uganda kama kitendo cha kiutu na kulingana na sheria ya kimataifa.

Msemaji wa jeshi la Uganda Meja Kiconco Tabaro amesema maafisa hao walirejeshwa pamoja na silaha zao na kuongeza kuwa wakimbizi walikuwa wakiendelea kuingia kupitia mpaka wa Uganda wakikimbia machafuko yanayoendelea mashariki mwa Kongo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo |  Wakimbizi walioko katika mji wa Minova
Maelfu ya watu walioyakimbia makazi yao kutokana na vita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Waasi wa M23 wameanzisha tena uasi katika eneo hilo lililozingirwa na makundi ya wanamgambo tangu mwaka 2022. Mwezi Juni, M23 waliukamata mji wa Kanyabayonga, na kuutumia kama lango la kuingia kwenye miji mingine ya jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo.

Soma pia: Kagame: Amani ya kikanda ni kipaumbele cha Rwanda

Juhudi za jeshi la Kongo za kuwarejesha nyuma waasi ziliongezeka mwaka uliopita likitumia droni na ndege za kivita, ingawa waasi hao wamezidi kujiimarisha na kudhibiti maeneo zaidi.

Soma pia:M23 wachukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Rutshuru 

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha zaidi ya watu milioni 1.7 kuyakimbia makazi yao, na kufanya jumla ya wakimbizi wa ndani kufikia milioni 7.2, hii ikiwa ni kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Soma pia:Uganda kuandaa mazungumzo kati ya DRC na makundi ya waasi