1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yakanusha kuwashikilia watoto raia wa Kenya

Lubega Emmanuel5 Mei 2022

Mamlaka za magereza nchini Uganda zimekanusha vikali madai kwamba zinawashikilia watoto ambao ni raia wa Kenya.

https://p.dw.com/p/4Asyy
Käfigfischen in Uganda
Picha: DW/Wambi Michael

 Kulingana na taarifa zilizochapishwa katika magazeti na vyombo vingine vya habari nchini Kenya, watoto hao wanne walikuwa miongoni mwa kundi la wavuvi 60 waliokamatwa wakiendesha uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa, watoto hao wanafunzi wa shule za sekondari na msingi, walikamatwa wakishiriki uvuvi haramu katika Ziwa Victoria upande wa Uganda.

Mahakama illwahukumu wavuvi wote 60 kifungo cha miezi sita baada ya kushindwa kulipa faini ya shilingi milioni moja na nusu za Uganda sawa na shilingi elfu hamsini za Kenya.

Taarifa zinaongezea kuwa juhudi za wazazi wa watoto hao kuwasiliana na mamlaka za Uganda waachiwe huru hazijazaa matunda yoyote.

Soma zaidi:Karibu watu 20 wamekufa katika ajali ya barabarani Uganda

Hata hivyo, msemaji wa magereza Frank Baine amekanusha madai kuwa wanaozuliwa kuhusiana na makosa hayo ni watoto na akaongezea kuwa hawahusiki hata kidogo na kukamatwa kwa wavuvi hao.

Wazazi, Wanaharakati haki za watoto waingilia kati

Kulingana na taarifa za wazazi, watoto hao wanne wamo katika madarasa ya kuandaliwa kufanya mitihani ya kitaifa.

Hii ndiyo inaleta mashaka na hasira kwamba wakiendelea kuzuiliwa katika magereza, hawataweza kuendelea na masomo yao.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa Ken Lukwago anashauri kuwa Uganda ingezingatia haki za watoto hao na kuwaachia huru kwa kuwapa onyo kali badala ya kuwasukuma gerezani.

Nairobi Unterricht mit Maske in Kenya
wanafunzi wakiwa kwenye mitihani NairobiPicha: Donwilson Odhiambo/ZUMA/picture alliance

Wavuvi hao 60  walikamatwa kwenye fukwe za Budalangi na Funyula miezi miwili iliyopita na kupekelekwa mahakamani mjini Kampala.

Soma zaidi:Mauaji yatikisa jamii za Kaskazini mwa Uganda

Jamaa za watoto zimenukuliwa zikitoa kilio kwa serikali ya Kenya iingilie kati. Juhudi za DW kupata tamko kutoka kwa kikosi cha jeshi cha kukabiliana na uvuvi haramu nchini Uganda hazijafanikiwa hadi wakati wa kuandaa taarifa hii.

Lakini kwa mtazamo wa mchambuzi Lukwago, suala hilo la kukabiliana na uvuvi haramu  linastahili kuhusisha mamlaka za pande zote mbili ili raia wa nchi moja wasidai kunyanyaswa.

Mara nyingi vifaa vya wavuvi haramu kwenye maziwa hukamatwa na kuchomwa moto kama njia mojawapo ya kuwazuia kufanya hivyo.

Stella Nyanzi: Mwanaharakati wa haki za binaadamu Uganda