1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Vyombo vya habari kuwasilisha majina ya wanaohojiwa

4 Agosti 2020

Vyombo vya utangazaji nchini Uganda vinahoji nia ya polisi kuwataka kuwasilisha majina ya wageni wanaoalikwa kwenye vipindi mbalimbali kabla ya kuwaruhusu hewani.

https://p.dw.com/p/3gOhs
Afrika Pressefreiheit l Uganda - Protest für Pressefreiheit - Daily Monitor Zeitung
Picha: Getty Images/AFP/M. Sibiloni

Kulingana na wanahabari, hii ni hatua moja ya kuvikandamiza vyombo vyao katika kipindi hiki cha uchaguzi, licha ya ukweli kwamba vyombo hivyo ndiyo njia kuu ya kufanyia kampeni kutoka na janga la covid-19.

Idhaa za redio na televisheni kote nchini zimeagizwa kutoa taarifa za watu wanaopanga kuwashirikisha kwenye vipindi mbalimbali. Katika taarifa hizo wakuu wa vituo watatakiwa kuelezea wanakotoka watu hao na ni nini ambacho watazungumzia.

Kwa mtazamo wa baadhi ya wanahabari hasa wale wanaoratibu vipindi, hii ni hila ya kuwasababisha baadhi ya watu kukataa mialiko ya vyombo vya habari kushiriki katika kutoa maoni yao kuhusu masuala kadha wa kadha.

Soma pia: Bobi Wine azindua chama kipya cha siasa kabla ya uchaguzi

Aidha ni njia mojawapo ya mkakati wa polisi kujiandaa kukabiliana na wafuasi wa wanasiasa wanaoandamana nao kwenda kwenye vituo vya redio na televisheni kuendesha kampeni zao.

Waandishi wa habari waitizama hatua hii ya Uganda kama ukandamizaji wa uhuru wa habari
Waandishi wa habari waitizama hatua hii ya Uganda kama ukandamizaji wa uhuru wa habariPicha: DW/Ole Tangen

Hata hivyo msemaji wa polisi Uganda Fred Enanga anasisitiza kuwa hatua hii imechukuliwa kuwawezesha kukabiliana watu wanaokiuka maagizo ya rais katika kipindi hiki cha kutotoka nje nyakati za jioni.

Polisi yakanusha madai kuwa inalenga kuwazuia wapinzani kuhojiwa na vyombo vya habari

Aidha amekanusha madai kuwa polisi hutumwa kwenye vituo vya redio kuwazuia wanasiasa wa upinzani wasishiriki kwenye vipindi vya redio na televisheni, hali ambayo imeshuhudiwa kwenye vituo kadhaa.

Lakini mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu Nicholas Opiyo anaonya kuwa katika msimu huu wa kuelekea uchaguzi mkuu pamoja na kipindi cha janga la covid-19, vyombo vya habari na jumuiya ya wanahabari kwa jumla watakabiliwa na wakati mgumu wa kukiukwa kwa haki zao za kujieleza.

Kwa wakati huu, wanasiasa wamo katika hekaheka za kuhamia vyama ambavyo wanamini vitawawezesha kupata ushindi. Chama tawala cha NRM na kile kikuu cha upinzani FDC vimepoteza wabunge kadhaa ambao wamejiunga na chama kipya cha NUP ambacho mgombea urais wake ni Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala