1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda kuwaadhibu wanaotema mate hadharani

11 Machi 2022

Wizara ya afya nchini Uganda imewasilisha bungeni muswada ambao unasema kuwa mtu atakayepatikana akitema mate sehemu za umma nchini atapata adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

https://p.dw.com/p/48KuD
Uganda | Coronavirus | Straßenhändler
Picha: Abubaker Lubowa/AA/picture alliance

Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyomo kwenye muswada wa afya ya umma ambao watu mbalimbali ikiwemo jumuiya ya madaktari wanapinga. Wanaelezea kuwa adhabu hiyo ni ya kidhalimu na itawaathiri wagonjwa ambao hawawezi kuepukana na kitendo hicho pale inapowabidi kufanya hivyo.

Kwa sasa muswada huo wa sheria ya kuwaadhibu watu wanaotema mate hadharani unachunguzwa na kamati ya bunge ambapo ikiwa utapitishwa ambaye hataweza kulipa faini ya shilingi milioni 3 za Uganda atahukumiwa kifungo cha miezi 12 gerezani.

Kulingana na serikali, tabia hiyo ina madhara makubwa kwa umma kwani husababisha maambukizi ya magonjwa ikiwemo kifua kikuu. Lakini pendekezo hilo limepokelewa kwa shutuma kali kutoka kwa raia mbalimbali wakishangaa na kuhoji jinsi mtu anavyoweza kuzuia kitendo cha kimaumbile.

Jumuiya ya madaktari nayo imejitokeza na kutoa taarifa kulipinga pendekezo hilo. Kwa mtazamo wao wa kiutaalamu ni sawa kabisa mtu kutema mate kwani ni njia mojawapo ya kujiondolea magonjwa au kutuliza mauvivu. Wamependekeza kuwepo na zoezi endelevu la kuwaelimisha watu kuhusu njia bora na wapi ni mahala salama mtu kutema mate badala ya kuwaadhibu watu. Aidha, wana mtazamo kuwa si rahisi kutoa ushahidi wa kuridhisha mahakamani kwamba mtu fulani ametema mate makusudi.

Afrika Uganda, Armut l Straßenkinder in Kampala
Mtaa wa jiji la KampalaPicha: DW/F. Yiga

Miongoni mwa mapendekezo yanayotolewa ni kwamba serikali kupitia idara za afya ya umma zitenge sehemu maalum ambapo watu wanaweza kutekeleza jambo hilo la kimaumbile sambamba na kuimarisha usafi wa mazingira ambao kwa sasa ni duni hasa katika mitaa ya mijini na pembezoni mwa miji.

Ni wazi kuwa kuepukana na tabia ya kutema mate ovyo ni jambo la kimaadili katika jamii nyingi, lakini pia katika jamii nyingine ni jambo la kawaida. Ni kwa msingi huu ndipo baadhi ya watu wanahimiza pasiwe na haraka ya kuadhibu bali watu wafahamu madhara husika.

Hivi karibuni wizara ya afya imejitokeza na mapendekezo kadhaa kuhusiana na njia ya kuimarisha usafi na afya za watu ikiwemo watu kuadhibiwa ikiwa hawajapata chanjo dhidi ya COVID-19. La sivyo watafungwa gerezani miezi sita au kutozwa faini ya shilingi milioni mbili pesa za Uganda.

Wataalamu wa afya pamoja na watetezi wa haki za binadamu pia wamepinga sheria hiyo iliyopendekezwa kama njia ya kuwashurutisha watu kupata chanjo hiyo. Muswada uliowasilishwa unalenga kurekebisha sheria ya mwaka 1935 kuhusu masuala ya afya ya umma.