1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Ufilipino, China zashutumiana Kusini mwa Bahari ya China

Angela Mdungu
31 Agosti 2024

China na Ufilipino zimeendelea kushutumiana baada ya meli za doria za mataifa hayo kugongana katika eneo la Sabina Shoal ambalo Ufilipino inaliita Escoda Shoal linalozozaniwa kwenye Bahari ya Kusini mwa China.

https://p.dw.com/p/4k8Oc
Ufilipino na China zimetuhumiana baada ya meli zao kugongana Kusini mwa Bahari ya China
Meli za China na Ufilipino zilipogongana Bahari ya Kusini mwa ChinaPicha: Philippine Coast Guard /AP Photo/picture alliance

Kila upande umekuwa ukimtuhumu mwenzake kwa kufanya vitendo vinavyohatarisha usalama katika eneo hilo. Kugongana kwa meli hizo ni tukio la tano kati ya majeshi ya wanamaji ya nchi hizo ndani ya mwezi Agosti. 

Soma zaidi: China yaionya Marekani juu ya kuiunga mkono Ufilipino katika mzozo wa bahari ya Kusini

Walinzi wa Pwani ya Ufilipino wanadai kuwa meli yao ya BRP Teresa Magbanua iliharibiwa pakubwa baada ya kugongwa mara tatu na meli ya China Jumamosi asubuhi.

Nayo China iliripoti kuwa meli ya Ufilipino iliyokuwa katika eneo hilo la mzozo iling'oa nanga na kuigonga meli ya China kwa makusudi  Jumamosi. Msemaji wa Walinzi wa Pwani wa China Liu Dejun ameitaka serikali ya Manila kuondoka haraka katika eneo hilo vinginevyo China itaichukulia hatua. Kwa upande wake balozi wa Marekani nchini Ufilipino amelaani ukiukwaji wa sheria ya kimataifa unaodaiwa kufanywa na China likiwemo tukio la leo la kuigonga meli ya Ufilipino.