1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi: Muungano wa kijeshi wa Marekani kulinda Hormuz?

11 Julai 2019

Marekani inasaka muungano wa kijeshi kulinda meli za mafuta kwenye milango bahari ya Hormuz na Bab El Mandab, lakini ni kwa kiasi gani muungano huo utafanikiwa? Soma uchambuzi wa Diana Hodali.

https://p.dw.com/p/3LviF
Spannungen in der Straße von Hormus
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Abulgasim

Kwa mujibu wa Mkuu wa Majeshi wa Marekani, Joseph Dunford, nchi hiyo itatoa ujuzi na uwezo wake kwenye masuala ya baharini kwa washirika hao, ili meli za zisizo za kijeshi ziweze kusindikizwa chini ya uangalizi wa jeshi la Marekani, bila kujali zinapeperusha bendera ya nchi yoyote ile iwayo.

Mlango Bahari wa Hormuz una umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa dunia, kwani ni hapo ndipo inapopitishwa robo nzima ya mafuta yanayosarifishwa kwa bahari ulimwenguni.

Ndicho kiungo kati ya wazalishaji wakubwa wa mafuta – Saudi Arabia, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuwait na Iraq – na masoko ya barani Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini. Ujia wa baharini wa Bab El Mandab upo baina ya Yemen na Djibouti na Eritrea, ambapo unaunda njia ya kusini kuelekea Bahari ya Sham, inayoungana na Mfereji wa Suez nchini Misri.

Kwa kuwa sehemu ya njia bahari ya Hormuz imo kwenye mpaka wa bahari wa Iran, Jamhuri hiyo ya Kiislamu imetishia mara kwa mara kuizuia njia hiyo. Katika wiki za hivi karibuni, hali ya wasiwasi kati ya Tehran na Washington imeongezeka, kwa sababu ya vikwazo vya Marekani baada ya kujiondosha kwenye mkataba wa nyuklia, na pia kwa sababu ya meli mbili za mafuta kushambuliwa kwenye eneo hilo mnamo mwezi Juni. 

Serikali ya Marekani ilituhumu Iran kuhusika na mashambulizi hayo, lakini serikali mjini Tehran ilikanusha tuhuma hizo. Muda mfupi baadaye, ndege isiyo rubani ya Marekani iliangushwa na Iran kwenye eneo hilo baada ya kuingia kwenye anga lake, na siku ya Jumatano (Julai 10), Iran ikaripotiwa kujaribu kuizuwia njia meli ya mafuta ya Uingereza.    

Washirika wanaotaka roho ya Iran

US Navy in Straße von Hormus
Mashua ya kijeshi ya Marekani kwenye mlango bahari wa Hormuz.Picha: picture-alliance/AP/K. Jebreili

Si Marekani pekee, hata mataifa ya Ghuba kama vile Saudi Arabia na Umoja wa Falme zinataka kurejesha nyuma ushawishi wa Iran kwenye eneo hilo kwa muda mrefu. Mtaalamu wa masuala ya Guba kwenye Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani, Sebastian Sons, anasema hii inalifanya suala la kuunda muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya Iran kuwa rahisi.

Hivi sasa Marekani inawasiliana na nchi kadhaa za eneo hilo, anasema Mkuu wa Majeshi Joseph Dunford, akiongeza kwamba katika siku za hivi karibuni patashuhudiwa mataifa kadhaa yenye nia ya kisiasa ya kujiunga na mpango huo. “Trump amelifanya suala la kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran kuwa sehemu ya kampeni zake na sasa hatua za kuitenga Iran zinasonga mbele,” anasema Dunford.

Kwa Saudi Arabia, sio tu kwamba ni adui mkubwa wa Iran, bali pia ni mshirika mkubwa wa Marekani kwenye eneo hilo. Kwa hivyo, utawala mjini Washington una uhakika kuwa ufalme huo wa Ghuba utajiunga na ushirika wa kijeshi, hasa katika wakati huu ambapo uhusiano binafsi kati ya Mrithi wa Ufalme Mohammed Bin Salman na Rais Donald Trump ulivyo wa ndani sana.

Mtaalamu wa masuala ya Guba kwenye Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani, Sebastian Sons, anasema kwa ukweli uhusiano baina ya mataifa haya mawili ni wa utegemezi zaidi kwa upande wa Saudia kuitegemea Marekani, kwa hivyo hakuna chochote kitakachoizuia Saudi Arabia kutekeleza matakwa ya Marekani kwenye hili.

Katika siku za karibuni, ufalme huo Katika siku za karibuni, ufalme huo uliongeza nguvu za mfumo wake wa kijeshi kwa kununuwa vifaa vya mamilioni ya dola kutoka Marekani.  

Kwa hivyo, sio tu Bin Salman ataweza kutoa msaada wa kimkakati, bali hata meli na ndege za kijeshi kwenye operesheni yoyote itakayoamuliwa.