1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Harris aongoza dhidi ya Trump uchunguzi wa maoni Marekani

24 Julai 2024

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amefungua mwanya wa asilimia mbili dhidi ya Mrepublican Donald Trump katika utafiti wa maoni ya kitaifa ya uchaguzi wa rais uliotolewa Jumanne.

https://p.dw.com/p/4ieKU
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris
Kamala Harris anapigiwa upatu kushinda uteuzi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa raisPicha: Kevin Mohatt/REUTERS

Ni utafiti wa kwanza kufanywa tangu Rais Joe Biden alipojiondoa katika kampeni ya kugombea kwa muhula wa pili. Harris ana asilimia 44 dhidi ya Trump aliye na asilimia 42 kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na Reuters na Ipsos. Ulifanywa katika siku mbili baada ya Biden kutangaza Jumapili kuwa anajiondoa kinyang'anyironi na kumpendekeza makamu wake wa rais.

Soma pia: Je, Harris ana uwezo wa kumshinda mgombea wa chama cha Republican Donald Trump?

Katika uchunguzi wa maoni wa wiki iliyopita, Harris mwenye umri wa miaka 59, na Trump, ambaye ana umri wa miaka 78, walikuwa wote na asilimia 44. Harris, anayepigiwa upatu na wengi kupata uteuzi wa chama cha Democratic, na ambaye anaendelea kuungwa mkono na vigogo na kupata michango, yuko nyuma ya mgombea wa Republican Trump kwa mwanya mdogo katika utafiti mwingine tofauti ambao pia ulitolewa Jumanne. Katika utafiti huo uliofanywa kwa pamoja na PBS/NPR/Marist siku ya Jumatatu, Trump ana asilimia 46 dhidi ya Harris aliye na asilimia 45 ya wapiga kura waliosajiliwa.