1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa madiwani katika wilaya sita nchini Burundi kurudiwa leo.

7 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CF61

Bujumbura:

Maafisa nchini Burundi wanasema mashambulio ya makombora ya usiku wa kuamkia leo katika vitongoji vya mji mkuu Bujumbura, yamelengwa kuvuruga marudio ya uchaguzi muhimu wa madiwani katika Wilaya sita baada ya vurugu zilizotokea Ijumaa iliopita. Jeshi la serikali linawalaumu waasi wa FNL kwa mashambulio hayo. Hakuna hasara ilioripotiwa zaidi ya uharibifu katika vituo vya kupigia kura katika mikoa ya Bujumbura vijijini na Buganza. Waasi hao pia walivishambulia vitongoji vya mji huo kwa risasi na makombora wakati wa uchaguzi wa madiwani ulipoanza Ijumaa iliopita . Maafisa wamesema upigaji kura utaendelea leo kama ilivyopangwa. Wakati huo huo matokeo ya awali baada ya uchaguzi siku ya Ijumaa yanaonyesha chama cha CNDD –FDD kimejinyakulia ushindi mkubwa. Tume ya uchaguzi inatazamiwa kutangaza matokeo rasmi kesho Jumatano. Hata hivyo tayari chama cha FRODEBU cha Rais Domicien Ndayizeye kimetaka uchaguzi mzima ubatilishwe, kikidai haukua huru na wa haki. Rais Ndayizeye amekishutumu chama cha CNDD-FDD akisema kiliwatisha wapiga kura.