1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Uchaguzi wa Jammu na Kashmir waleta matumaini eneo tete

17 Septemba 2024

India inaandaa uchaguzi wa kwanza katika muongo mmoja kwenye mkoa wa Jammu na Kashmir. Wakaazi wa eneo hilo wana matumaini ya tahadhari katikati mwa ghasia zisizoisha.

https://p.dw.com/p/4kjAh
Mkoa wa Kashmir | Uchaguzi wa mikoa
Wapiga kura wajadili matumaini ya uchaguzi na hofu inayoikabili Kashmir katika uchaguzi wa kwanza wa kikanda katika muongo mmoja. Wapiga kura wanatumai uchaguzi huo utaleta maendeleo yanayohitajika katikati mwa ongezeko la ukosefu wa ajira.Picha: DW

Katika mkutano wa kampeni kusini mwa Kashmir, Shameema Jan mwenye umri wa miaka 45 anapaza sauti yake na kuungana na makumi ya wanawake wengine katika kuimba nyimbo za kitamaduni za kuunga mkono mgombea wao wanayempendelea kabla ya uchaguzi wa kikanda wa Jammu na Kashmir unaotarajiwa kuanza Jumatano.

Matumaini waliyonayo wanawake hawa ni rahisi. Wanataka mwakilishi, ikiwezekana mwanamke, ambaye anaweza kushughulikia matatizo yao ya kila siku, kama vile uhaba wa maji kijijini, kufungwa kwa vijana wao katika jela nje ya Kashmir, na suala linaloongezeka la ukosefu wa ajira kwa vijana katika eneo hilo lenye Waislamu wengi linalodhibitiwa na India.

Kwao, mgombea huyu ni Iltija Mufti, binti wa Waziri Mkuu wa zamani Mehbooba Mufti, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa serikali ya Jammu na Kashmir hadi 2018.

"Yeye ni mdogo na ana nguvu," Jan aliiambia DW kuhusu Iltija Mufti. "Ikiwa tutampigia kura, atatusikiliza. Tuna vijana wengi katika jela nje ya Kashmir, na tunataka waachiliwe," Jan aliongeza, wakati Mufti akihutubia mkutano huo akiwa juu ya gari lake.

"Uchaguzi huu unaweza kubadilisha hali yetu," Jan alisema, huku wanawake waliomzunguka wakikubali kwa kutikisa vichwa.

Mkoa wa Kashmir |Uchaguzi wa mikoa
Wapigakura wakimskiliza mgombea wakati wa kampeni huko Kashmir.Picha: DW

Wanaopigania kujitenga wavikabili vyama vikuu kwenye sanduku la kura

Jammu na Kashmir inatarajia kufanya uchaguzi wake wa kwanza wa mabunge ya kikanda katika muongo mmoja. Kura ya mwisho kama hii ilifanyika mwaka wa 2014 wakati Chama cha Bharatiya Janata cha Waziri Mkuu wa India Narendra Modi (BJP) na Peoples Democratic Party (PDP) kilipounda serikali ya mseto.

Soma pia: Mahakama kuu ya India yaidhinisha mwisho wa hadhi maalum ya Kashmir

Lakini muungano huo ulivunjika mnamo 2018 wakati BJP iliondoa uungaji mkono wake na New Delhi ikachukua udhibiti wa moja kwa moja wa mkoa huo uliokumbwa na vurugu za kujitenga.

Sasa, kura inayokuja inatoa nafasi kwa watu wa Kashmir kuchagua serikali mpya baada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa. Pia ni uchaguzi wa kwanza wa kikanda tangu eneo hilo kupokonywa hadhi yake maalum na kugawanywa katika maeneo mawili ya muungano wa Jammu na Kashmir na Ladakh.

Vyama vya kikanda kama vile Jammu and Kashmir National Conference (NC) na PDP, pamoja na vyama vikubwa vya kitaifa kama vile BJP na Indian National Congress (INC), vyote vinashiriki uchaguzi huu.

Lakini pia kuna watu wengi wanaotaka kujitenga wanaogombea kama watu huru, wakiashiria mabadiliko makubwa kutoka msimamo wao wa awali wa kususia uchaguzi kabisa.

Kundi la Kiislamu lililopigwa marufuku lashirikiana na 'Mhandisi Rasheed'

Uchaguzi wa kitaifa uliofanyika msimu wa machipuko mwaka huu tayari umedokeza juu ya kizazi kipya cha viongozi, akiwemo Abdul Rasheed Sheikh, anayejulikana zaidi kwa wafuasi wake kama "Mhandisi Rasheed."

India | Mhandishi Rasheed
Mhandishi Abdul Rasheed Sheikh (kushoto) na wafuasi wake wakiandamana mjini Srinagar, mjii mkuu wa Kashmir. Rasheed anawania katika uchaguzi wa mkoa wa Kashmir.Picha: Farooq Khan/dpa/picture alliance

Mhandisi huyo wa zamani wa ujenzi aligombea ubunge wa kitaifa akiwa jela baada ya kuzuiliwa kwa tuhuma za kufadhili ugaidi. Bado alifanikiwa kupata ushindi mnono. Chama chake cha Awami Itehad (AIP) kinatarajiwa kutoa changamoto kali kwa vyama vya jadi vya kisiasa katika uchaguzi ujao.

"Tunashiriki katika uchaguzi kwani hatutaki kuishi kwa hofu ya kudumu," Manzoor Ahmad, mshiriki wa mkutano wa wafuasi wa AIP katika mji wa Kashmiri wa Tral aliiambia DW. "Tulijitokeza kwa wingi kumsikiliza Rasheed kwa sababu hotuba zake zinaakisi mawazo na fikira zetu,” aliongeza.

Soma pia:Kwanini India inazozana na Pakistan juu ya mkataba wa kihistoria? 

Sheikh alipewa dhamana ya muda mwezi Septemba, na kumruhusu kushiriki katika kampeni. Mmoja wa wafuasi wake, Atiqa Jan, aliiambia DW mwanawe yuko jela na alitaka atoke nje.

"Mwanangu amekuwa gerezani kwa mwaka mmoja uliopita na nilitaka kumweleza haya Rasheed kwani anaelewa uchungu wangu,” alisema.

Chama cha AIP cha Sheikh pia kimeunda muungano wa kabla ya uchaguzi na kundi lililopigwa marufuku la Jamat-e-Islami, ambalo wagombea wake wanashiriki rasmi kama watu huru katika uchaguzi ujao.

BJP yapambana kupata uungwaji mkono wa kisiasa Kashmir

Chama cha BJP cha Waziri Mkuu Narendra Modi kimekuwa kikipambana kupata kuungwa mkono katika bonde la Kashmir lenye Waislamu wengi. Lakini kina tajiriba kubwa ya wapiga kura katika eneo la Jammu lenye Wahindu wengi. 

Zaidi ya hayo, Jammu ni eneo bunge muhimu kwa BJP ambapo inaweza kutumia matamshi yake ya utaifa, masuala ya usalama, na ahadi za miradi ya maendeleo.

Soma pia: Kashmir: Khan aapa 'kupambana hadi mwisho'

Mnamo Septemba 14, Waziri Mkuu Modi aliuambia mkutano wa kisiasa katika wilaya ya Doda ya Jammu kwamba BJP imeleta neema katika mkoa mzima. "Sisi na wewe kwa pamoja tutaifanya Kashmir kuwa sehemu salama na yenye ustawi wa nchi," alisema.

Pia aliahidi kwamba ugaidi ulikuwa "unavuta pumzi yake ya mwisho katika Jammu na Kashmir" - licha ya vurugu za kujitenga. Lakini viongozi wa kisiasa wa eneo hilo wanapinga madai ya BJP ya mabadiliko wanayoyataja kuwa "uzushi."

"Ni jambo la aibu kwa BJP ambayo imekuwa ikisema hali imeboreka, lakini hawakuweza kuandaa uchaguzi katika Jammu na Kashmir katika miaka 10 iliyopita. Watu wamekasirika, wanakosa hewa," Waziri Mkuu wa zamani wa Kashmir Mehbooba Mufti alisema.

Fursa ya kupinga mageuzi ya New Delhi?

Serikali mpya iliyochaguliwa itakuwa na mamlaka yaliopunguzwa kwa sababu ya hali ya sasa ya Jammu na Kashmir kama Eneo la Muungano baada ya mabadiliko ya kisiasa mwaka wa 2019.

Maeneo mengi muhimu, kama vile sheria na utulivu na masuala ya ardhi, yanasalia chini ya udhibiti wa New Delhi ambapo serikali ya mkoa haiwezi kufanya mabadiliko yoyote.

"Uchaguzi ni muhimu na sio muhimu kwa wakati mmoja," Profesa Noor Muhammad Baba, mchambuzi wa kisiasa wa kikanda, aliiambia DW.

"Una umuhimu kwa sababu unafanyika baada ya muda mrefu na watu watapata kuchagua wawakilishi wao, na pia kwa sababu hii itatumika kama ujumbe wa jinsi watu wanavyokasirika na kuchukia mabadiliko."

Lakini anaonya mabadiliko hayo hayo yanamaanisha kuwa serikali itakuwa na "nguvu kidogo."

"Sasa watu wataamua iwapo wanasimamia mabadiliko au dhidi yake," alisema.