1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Israel: Benjamin Netanyahu awania muhula wa nne

Zainab Aziz Mhariri; Yusuf Saumu
17 Septemba 2019

Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi nchini Israel leo Jumanne, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anawania muhula wa nne lakini anakabiliwa na ushindani mkali.

https://p.dw.com/p/3PiPF
Israel | Parlamentswahlen 2019 | Wahllokal
Picha: Reuters/C. Kern

Watu nchini Israel wameanza kupiga kura katika uchaguzi utakaoamua iwapo Waziri Mkuu wa sasa Benjamin Netanyahu ataendelea kuwemo madarakani huku akiwa katika wasiwasi wa kufikishwa  mahakamani kujibu tuhuma za kuhusika na ufisadi. 

Waziri Mkuu huyo ambaye amekuwamo madarakani kwa muda mrefu zaidi kuliko mwengine yeyote anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa jenerali mstaafu Benny Gantz. Chama cha jenerali huyo mstaafu cha Buluu na Nyeupe kiko sambamba na chama  cha Netanyahu cha Likud.  Hata hivyo vyama hivyo vitalazimika kuunda mseto na vyama  vidogo itakapobidi kuunda serikali. Leo asubuhi Rais wa Israel Reuven Rivlin alipiga kura katika mji wa Jerusalem na alisema kuwa leo ni israel inasherehekea demokrasia.

Waziri Mkuu Netanyahau amejaribu kujinadi kuwa yeye ni kiongozi mwenye sifa za kipekee za kuiongoza  nchi katika nyakati za changamoto. Lakini mshindani wakejenerali mstaafu Benny Gantz anamzungumzia  Netanyahu kuwa Waziri Mkuu anayeigawanya nchi na pia mwanasiasa anayeandamwa na kashfa. Gantz anajinadi kama mtu mtulivu na mwadilifu.

Gantz alipokwenda kupiga kura alisema waisraeli leo hii wanapiga kura ya mabadiliko. Kiongozi huyo wa chama cha Bluu na Nyeupe, amesema chama chake kitafanikiwa kuleta matumaini, bila rushwa na bila kuwepo misimamo mikali.

Kushoto: Kiongozi wa chama cha Buluu na Nyeupe Benny Gantz. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Kushoto: Kiongozi wa chama cha Buluu na Nyeupe Benny Gantz. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Netanyahu na jenerali huyo mstaafu leo wanapambana kwa mara ya pili mnamo mwaka huu baada ya kutoka sare katika uchaguzi uliofanyika mnamo mwezi wa Aprili. Hata hivyo Waziri Mkuu Netanyahu ameonyesha matumaini ya kuendelea kuwamo madarakani kutokana na kuungwa mkono na washirika  wake wa jadi wa vyama vya mrengo mkali wa kiyahudi vinayvodhibiti viti vingi bungeni,  lakini mshirika wake  wa hapo awali ambaye sasa amekuwa hasimu wake Avigdor Lieberman alikataa kujiunga na serikali mpya  ya mseto na hivyo kupungza viti vya serikali ya Netanyahu bungeni. Waziri mkuu huyo alilazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya.

Uchunguzi wa maoni umebainisha kwamba matokeo ya uchaguzi wa leo yanatarajiwa kuwa kama ya hapo  awali. Chama cha bwana Liebermann ndicho kinachotarajiwa kuwa muhimu kabisa katika hesabu za kuunda  serikali. Baada ya kupiga kura bwana Lieberman alisisitiza ahadi ya kuwezeshwa kuundwa kwa serikali ya umoja baina ya chama cha Bluu na Nyeupe na chama cha Likud. Amesema haitafanyika duru ya tatu ya uchaguzi.

Katika uchaguzi  wa leo mfungamano wa vyama vinavyowawakilisha waarabu wa Israel pia vinatarajiwa kuwa muhimu kama jinsi  iliyvokuwa katika uchaguzi wa mwaka wa 2015 ambapo vilishika nafasi ya tatu  kwa idadi ya viti  bungeni. Na ikiwa utabiri utakuwa sahihi vyama hivyo vinaweza  kuzima ndoto ya Waziri Mkuu Netanyahu ya kuchaguliwa  kwa mara ya tano.

Vyanzo:/AP/DPA/AFP