1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge na madiwani waanza Burundi

Mjahida 29 Juni 2015

Wananchi wa Burundi wanapiga kura katika uchaguzi wa bunge uliosusiwa na vyama vya upinzani.Uchaguzi huo unafanyika licha ya Jumuiya ya kimataifa kutoa mwito uakhirishwe kutokana na hali mbaya ya usalama.

https://p.dw.com/p/1Fotg
Mafanyakazi wa tume ya uchaguzi akitayarisha vijisanduku vya kupigia kura
Mafanyakazi wa tume ya uchaguzi akitayarisha vijisanduku vya kupigia kuraPicha: Reuters/P. Nunes dos Santos

Raia wa Burundi wapatao milioni 3, 842 728 wanatarajiwa kupiga kura kuwachaguwa madiwani 640 wa tarafa 129 zinazo unda nchi ya Burundi sawa na madiwani 15 katika kila tarafa.

Katika uchaguzi huu pia wabunge 106 watakaounda bunge la taifa watachaguliwa. Upigaji kura unafanyika katika vituo elfu 11, 493 vilivyotengwa nchi zima. Katika mji mkuu Bujumbura, upigaji kura uliotarajiwa kuanza saa 12 asubuhi ulianza kuchelewa katika baadhi ya vituo.

Katika sehemu nyingine maafisa wa tume ya uchaguzi wakionekana kuanza kwanza kwa kuwakumbusha wapiga kura utaratibu unao stahili kutiliwa maanani.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Pierre Claver Ndayicariye alitangaza kubadilishwa vituo vya kupigia kura asubuhi ya Jumatatu kwa kile alichosema kuwa ni sababu za kiusalama.

Wafanyakazi wa tume ya uchaguzi Burundi wakisubiri wapiga kura katika vituo vya kupigia kura vilivyokuwa havina watu
Wafanyakazi wa tume ya uchaguzi Burundi wakisubiri wapiga kura katika vituo vya kupigia kura vilivyokuwa havina watuPicha: picture-alliance/EPA/KUROKAWA

Mwenyekiti huyo aliwaagiza waangalizi ambao wote ni kutoka mashirika ya kitaifa isipokuwa tu tume ya Umoja wa mataifa ya kufuatilia uchaguzi Menub na wale kutoka vyama vya CNDD FDD na Uprona kusalia vituoni tangu kufunguliwa hadi zowezi litakapo hitimishwa.

Aimable Niyonkuru, Mkaazi wa Bujumbura mwenye umri wa miaka 20 aliyewahi kuwa mfuasi mkubwa wa chama cha rais Nkurunziza CNDD-FDD, amesema hatashiriki katika uchaguzi huo wa kuwachagua wabunge na madiwani kwa sababu rais Nkurunziza hajaimarisha uchumi wa nchi au kutekeleza kile alichokiahidi kukifanya katika uongozi wake.

"Nimevunjika moyo sana kwa kila wanasiasa wanachokifanya, nadhani sio wazalendo kabisa," alisema Aimable Niyonkuru.

Uchaguzi wafanyika wakati hali ya usalama ikiwa sio nzuri

Uchaguzi huo unafanyika wakati milio ya risasi na maguruneti takriban mawili vikisikika katika mji mkuu Bujumbura usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mtu mmoja aliyeshuhudia amesema mripuko mmoja ulitokea katika mtaa wa Musaga Jumatatu asubuhi, huku gazeti linalojitegemea la Iwacu likinukuu tovuti ya polisi iliyosema miripuko miwili ilitokea katika wilaya ya Mayuyu kilomita 25 Kusini Mashariki mwa Bujumbura.

Baadhi wa wakaazi wa Burunmdi walioandamana kumpinga rais Nkurunziza kugombea Urais kwa muhula wa tatu
Baadhi wa wakaazi wa Burunmdi walioandamana kumpinga rais Nkurunziza kugombea Urais kwa muhula wa tatuPicha: Reuters/G. Tomasevic

Shambulio hili limefuatia jengine lililotokea wiki iliyopita mjini humo lililosababisha mauaji ya watu wanne huku wengine wengi wakijeruhiwa. Msemaji wa Polisi hakuweza kupatikana mara moja kutoa maoni yake juu ya tukio hili.

Licha ya kuwepo ukosoaji mkuwa wa hatua ya Nkurunziza kutoka jamii ya Kimataifa serikali imeendelea na uchaguzi huo wa bunge pamoja na kuendelea na mipango ya kuandaa uchaguzi wa rais mnamo Julai 15, hii ikiangaliwa kama hatua ambayo huenda ikachochea mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu kumalizika kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005

Mataifa ya Afrika hayatatuma waangalizi

Mataifa ya Kiafrika na wafadhili wa Magharibi waliitisha mazungumzo kati ya pande mbili hasimu serikali na upinzani, pamoja na kutaka uchaguzi uahirishwe, wakidai kuwa vyombo vya habari ni lazima vikubaliwe kufanya kazi kwa uhuru pamoja na masuala mengine kuzingatiwa ili kutoa nafasi ya kufanyika uchaguzi wa haki.

Hapo Jumapili Umoja wa Afrika ulisema hautatuma waangalizi katika uchaguzi huo kwasababu hauna imani kwamba uchaguzi utakuwa wa huru na haki. Kwa upande mwengine Marekani na mataifa ya Umoja wa Ulaya yamezuwiya misaada yao nchini Burundi na kutishia kuwawekea vikwazo watu watakaobainika kuchochea vurugu.

Viongozi wa Jumuiya wa Afrika Mashariki wakikutana kujadili mgogoro wa Burundi
Viongozi wa Jumuiya wa Afrika Mashariki wakikutana kujadili mgogoro wa BurundiPicha: DW/H. Bihoga

Huku hayo yakiarifiwa zaidi ya watu 125,000 au zaidi ya asilimia moja ya idadi ya watu milioni 10 nchini humo wamekimbia katika mataifa jirani na kuongeza wasiwasi katika eneo hilo lililo na historia ya mapigano ya kikabila hasaa nchini Rwanda iliopitia mauaji ya Kimbari mwaka 1994.

Nkurunziza, aliyewahi kuwa kiongozi wa waasi wa jamii ya waliowengi Wahutu dhidi ya jamii ya wachache watutsi wakati wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe amekuwa akitegemea maeneo yanayomuunga mkono katika amaeneo ya mashinani katika uchaguzi huu.

Mwandishi/Amida Issa/Amina Abubakar/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga