1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi DRC wacheleweshwa kwa wiki moja

Daniel Gakuba
21 Desemba 2018

Tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeahirisha kwa wiki moja uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 23 na kuuhamishia tarehe 30 Desemba, 2018. Hatua hiyo imelalamikiwa na wagombea wa upinzani.

https://p.dw.com/p/3ATBW
Demokratische Republik Kongo - Wahl: Corneille Nangaa Yobeluo
Corneille Nangaa Yobeluo, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi DRCPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

Uamuzi wa kuahirisha uchaguzi huo umetangazwa Alhamis jioni mjini Kinshasa, na mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, Corneille Nangaa.

''Tunatangaza kwamba uchaguzi wa rais, bunge na wabunge wa majimbo utafanyika tarehe 30 Desemba 2018. Mabadiliko yanayosababishwa na hatua hiyo yatapewa ufumbuzi usiku huu,'' amesema Nangaa katika mkutano na waandishi wa habari, baada ya mashauriano na wagombea urais katika uchaguzi huo.

Sababu zilizotolewa kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni pamoja na kuunguwa kwa ghala vya kuhesabia kura mjini Kinshasa, ghasia zilizofanyika wakati wa kampeni, na hofu ya kuenea kwa maradhi hatari ya Ebola Mashariki mwa nchi.

Wapinzani walalamika

Mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, Martin fayulu tayari ameipinga hatua hiyo, akimshutumu mkuu wa tume ya uchaguzi kukosa uwajibikaji.

Feuer zerstört Wahlgeräte in Kinshasa
Kuungua kwa ghala la vifaa vya uchaguzi kumetajwa kama sababu mojawapo ya kusogezwa kwa tarehe ya uchaguziPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

''Hatua hii ya kuahirishwa kwa uchaguzi ni alama tosha kwamba kuna kasoro katika maandalizi ya uchaguzi huo. Corneille Nangaa ni wapi ameweka kiburi chake leo, alikuwa akimkejeli kila mtu akisisitiza kwamba kwa vyovyote vile uchaguzi utafanyika tarehe 23 Desemba; leo ukomo uko wapi? Nafikiri Nangaa ni lazima abebe dhamana yake.'' Amesema Fayulu baada ya tangazo la Nangaa.

Chama tawala kimeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya tume ya uchaguzi ya kuahirisha uchaguzi. Kikaya Bin Karubi, mshauri wa kidiplomisa wa Rais Joseph Kabila amesema kwamba ni jambo la kusikitisha kwamba kampeni yao imesitishwa mapema, lakini akaongeza kwamba wanaheshimu uamuzi huo wa tume ya uchaguzi. 

Hali iliendelea kuwa tulivu mjini Kinshasa baada ya tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi, lakini baadhi ya maduka yalifunga milango yake kwa tahadhari, yakiogopa kutokea machafuko.

Wananchi wasikitika, wataka uchaguzi wenye uwazi

DR Kongo Martin Fayulu
Martin Fayulu, mgombea wa upinzani aliyekosoa hatua ya kuahirisha uchaguziPicha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Kwa upande wao wananchi wameomba kuweko na uchaguzi wa kuaminika katika mazingira yenye uchaguzi, ingawa wamesikitishwa na hatua hiyo ya kuahirisha uchaguzi.

''Tulikuwa tayari kupiga kura Jumapili tarehe 23 Desemba. Kuahirishwa huku tunakuchukulia kama mapungufu upande wa serikali.'' Amesema kijana mmoja aliyezungumza na DW mjini Kinshasa.

''Tulikuwa tunapendelea uchaguzi ufanyike kama ilivyopangwa, usiahirishwe na kupelekwa mbali, kwani yapo matatizo mengine mengi.'' Amelalamika mwingine.

Hatua hiyo ya kuuahirisha uchaguzi imekuja baada ya tume kufanya mashauriano na wagombea wote 21 waliojitosa katika kinyang'anyiro cha urais.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa

Mhariri: Daniel Gakuba