1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchafuzi wa mazingira ni hatari kuliko vita, maafa na njaa

20 Oktoba 2017

Uchafuzi wa mazingira unaua watu wengi zaidi kila mwaka kuliko hata vita, maafa na baa la njaa, pamoja na hata uvutaji sigara na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa kiuchumi, kulingana na utafiti.

https://p.dw.com/p/2mFR1
Kraftwerk Oberhausen Wasserdampf Abgase
Picha: Getty Images/L. Schulze

Karibu nusu ya vifo vya jumla hutokea katika nchi mbili tu, kwa mujibu wa utafiti uliotolewa katika jarida la matibabu la Lancet.

Kulingana na utafiti huo, moja ya kila sita ya vifo milioni 9 vya mapema kote duniani katika mwaka wa 2015, vinaweza kuhusishwa na magonjwa yanayosababishwa na sumu katika hewa au maji.

Aidha ripoti hiyo inasema uchafuzi wa hewa ndio sababu kuu ya vifo hivyo, ukihusika na milioni 6.5 ya vifo, ukifuatiwa na uchafuzi wa maji, ambao uliwaua watu milioni 1.8.

Makisio ya vifo milioni 9 vya mapema, ni mara moja na nusu juu kuliko idadi ya watu waliouawa kutokana na uvutaji sigara, na mara tatu idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI, kifua kikuu au TB na malaria kwa pamoja. Pia ni mara 15 idadi ya watu waliouawa katika vita au aina nyingine za vurugu.

Asilimia tisini na mbili ya vifo vinavyotokana na uchafuzi wa mazingira vilitokea katika nchi zinazoendelea zenye mapato ya chini au ya kati, huku India ikiongoza kwenye orodha kwa milioni 2.5, ikifuatiwa na China , milioni 1.8.

Indien Luftverschmutzung Diwali
Mji wa New Delhi wapiga marufuku baruti katika sherehe za Diwali mwaka huu kupunguza uchafuzi wa hewaPicha: picture-alliance/dpa/M.Swarup

Gharama za Kiuchumi

Ripoti hiyo pia imeonyesha  gharama kubwa zinazotokana na vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, magonjwa na ustawi, na kukadiria gharama hizo zinafikia dola bilioni 4.6 katika hasara za kila mwaka - au sawa na  asilimia 6.2 ya uchumi wa dunia.

"Kile ambacho watu hawatambui ni kwamba uchafuzi wa mazingira unaathiri uchumi. Watu ambao ni wagonjwa au wafu hawawezi kuchangia katika uchumi, wanahitaji kutunzwa."  Amesema mmoja wa waandishi wa utafiti, Richard Fuller, ambaye ni mkuu wa shirika la kimataifa linalochunguza maswala ya uchafuzi wa mazingira la Pure Earth.

Kulingana na utafiti huo, mzigo wa kifedha pia unaathiri nchi maskini zaidi, na nchi za kipato cha chini zikitoa asilimia 8.3 ya GNP yao ili kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, ikilinganishwa na asilimia 4.5 katika nchi tajiri.

Wahariri wa Lancet, Pamela Das na Richard Horton walisema, ripoti hii imekuja wakati wa hofu " wakati shirika la ulinzi wa mazingira la serikali ya Marekani likiongozwa na Scott Pruitt likikandamiza kanuni imara za mazingira.

Pruitt alitangaza mwezi huu kuwa Marekani, msababishaji mkubwwa wa uchafuzi wa hewa na gesi chafu, kwamba itajitoa nje kwenye mpango wa kuzalisha hewa safi ulioundwa na aliyekuwa Rais Barack Obama.

Das na Horton wanasema matokeo haya yanapaswa kuwa "wito wa kutaka hatua zichukiwe.”

Mwandishi: Fathiya Omar/DW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman