1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UCDP: Idadi ya waliouwawa kwa migogoro duniani imepanda

7 Juni 2023

Kundi moja la utafiti la Sweden limeripoti kwamba idadi ya watu waliuwawa katika vita na migogoro ilikaribia kupanda mara mbili, na kufikia kiwango kikubwa tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/4SJOi
Äthiopien Mekelle | Tigray-Streitkräfte  Übergabe von  Waffen an äthiopische Armee
Picha: Million Hailessilasie/DW

Watafiti kutoka mpango wa kushughulikia masuala ya migogoro UCDP, katika chuo kikuu cha Uppsala nchini Sweden, wamesema watu takriban 237,000 waliuwawa katika migogoro ya kijeshi mwaka 2022. Watafiti hao pia wamesema kwamba, idadi hiyo inaonyesha mauaji hayo yameongezeka kwa asilimia 97 ikilinganishwa na mwaka 2021, huku wakiongeza kuwa idadi ya migogoro inayoendelea duniani inabakia kuwa juu zaidi.

Watafiti hao sasa wanapanga kuchapisha utafiti wao katika jarida la utafiti wa amani mwezi Julai. Shawn Devis mtaalamu katika kundi hilo amesema huku viwango vya migogoro vikiripotiwa kushuka nchini Yemen na  Afghanistan hali nchini Ukraine na Ethiopia imeendelea kuwa mbaya.

Watu wahamishwa kufuatia shambulizi kusini mwa Ukraine

Devis amesema vita hivyo vya Ukraine na Ethiopia vimesababisha mauaji ya watu 180,000 Idadi inayokadiriwa kuwa ndogo na inayohofiwa kuongezeka zaidi kufuatia habari zinazoendelea kujitokeza.

Urusi ilimvamia jirani yake Ukraine miezi 15 iliyopita. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia kati ya Viongozi wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF na serikali vimekuwa vikipamba moto tangu mwishoni mwa mwaka 2020 na kumalizika mwezi Novemba mwaka 2022, kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanzishwa kwa mazungumzo ya amani.

Hali ya utulivu yarejea katika jimbo la Amhara, Ethiopia

Davies anasema japo watu wanaamini kwamba vita vya Urusi nchini Ukraine ndivyo vita vibaya zaidi kutokea mwaka 2022 lakini watu wengi ndio wameuwawa nchini Ethiopia kuliko Ukraine.

Kufuatia data za kundi la UCDP, Taasisi ya otafiti wa amani ya Norway pia lilisema kwamba zaidi ya watu 100,000 waliuwawa nchini Ethiopia mwaka 2022 na zaidi ya watu 81,000 waliuwawa nchini Ukraine.

Chanzo: dpa