1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubadhirifu wa huduma za dawa katika hospitali za Tanzania

1 Machi 2021

Hospitali zipatazo 28 za mikoa Tanzania bara zimegundulika kukumbwa na ubadhirifu wa huduma za dawa na matibabu mengine hali inayomlazimu waziri wa afya kuamuru viongozi wote kwenye hospitali hizo wafanyiwe mabadiliko.

https://p.dw.com/p/3q43k
Venezuela Gesundheitssystem
Picha: picture-alliance/dpa/M. Gutierrez

Ripoti iliyotolewa na waziri wa afya, Dr Dorothy Gwajima inaonyesha sehemu kubwa wasimizi wa hospitali hizo kwa njia moja ama nyingine wamehusika kuzorotesha huduma za afya kwa kushindwa kusimamia ipasavyo mgawanyo wa dawa na vipimo.

Mathalani katika baadhi ya maeneo licha ya serikali kuu kupelekwa dawa na vipimo kwa wakati,lakini huduma zilizotolewa hazikukidhi viwango hali ambayo ilizidisha manung'uniko kutoka kwa wananchi.

Kugundulika kwa hali hiyo kimefuatia kukamilisha kazi kwa timu maalumu ya wataalamu iliyoundwa na waziri huyo iliyofanya kazi kwa kipindi kufupi na hatimaye kubaini mwenendo huo. Wazairi Dr Gwajima amedai kuwa, ubadhilifu huo unaitia doa sekta ya afya ambayo imekuwa ikiongezewa bajeti yake kila inapohitajika kufanya hivyo.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015- 16 bajeti ya sekta ya afya iliongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi kufikia bilioni 270. Ongezeko hilo linahusisha pia, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na uboreshaji wa hospitali za rufaa na uongezwaji wa vifaa tiba.

Madaktari wapya kuajiriwa kukabiliana na uhaba wa madaktari

Symbolbild Apotheke Äquatorialguinea
Picha: imago/imagebroker

Hivi karibuni pia serikali ilitangaza kuajiri madaktari wapya kadhaa ili kukabiliana na pengo la uhaba wa wataalamu wa kada hiyo, hasa katikamaeneo yaliyoko pembezoni na miji mikubwa ambako kumekuwa na chimbuko kubwa la magonywa yasiyokuwa ya kuambukizwa na yale yaambukizwayo.

Kulingana na Waziri Dk Gwajima, wizara yake imepanga kufanya uchunguzi mwingine kama huu, safari hii maeneo yatakayotupiwa macho ni pamoja na hospitali za rufaa mpaka zile za taifa kwa shabaha hiyo hiyo moja kubaini mianya inayofisadi huduma za matibabu kwa wananchi.

Sekta ya afya ni miongoni mwa sekta zinazotupiwa lawama mara kwa mara na wananchi wengi kutokana na urasimu pamoja na ucheleweshaji wa utoaji wa huduma za matibabu.

Makundi ya wazee ni miongoni mwa wale wanaoibua lawama hizo kwa madai kuwa licha ya kuahidiwa kupatiwa matibabu bure,lakini wakati mwingine wanalazimika kuingia mifukoni mwao kwa ajili ya kununua dawa.

Mwandishi: George Njogopa