1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tundu Lissu atangaza nia ya kugombea urais Tanzania

8 Juni 2020

Aliekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu, ametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2020 nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3dS0v
Tundu Lissu Abgeordneter und Oppositionspolitiker überlebte ein Attentat in Tansania
Picha: DW

Tundu Lissu alietangaza nia kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, ameishutumu vikali serikali inazoongoywa na chama cha mapinduzi kwa kile alichokitaja kuwa kutozingatia utawala wa kisheria pamoja na kurudisha nyuma uchumi na democrasia ya taifa hilo la Afrika mashariki.

Tundu Lissu ametangaza nia yake akiwa katika ardhi ya ugenini nchini Ubelgiji ambako anapokea matibabu baada ya shambulio la kupigwa risasi kadhaa na watu wasiojulikana katika mji mkuu Dodoma. Miongoni mwa hoja alizozipa kipaumbele wakati akiweka hadharani nia yake ya kugombea urais ni kuzifutilia mbali sheria zote alizoziita kandamizi na zinazotumika katika kuminya uhuru wa raia.

Mwanasiasa huyo ambae pia ni mwanasheria amesema, takriban miaka mitano sasa utaratibu wote wa haki za binadamu umeonekana kukiukwa kwa kiwango kikubwa, kutokana na mfululizo wa matukio ya utekwaji na watu kupotea, huku hali ya wananchi kiuchumi ikiendelea kuzorota kwa kiwango cha hali ya kutafakarisha.

Lissu: Serikali yatumia mbinu mbalimbali kuua mfumo wa vyama vingi

Mnamo mwaka 2017, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi kadhaa na watu wasiojulikana nchini Tanzania. Tangu wakati huo, mwanasiasa huyo amekuwa ughaibuni.
Mnamo mwaka 2017, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi kadhaa na watu wasiojulikana nchini Tanzania. Tangu wakati huo, mwanasiasa huyo amekuwa ughaibuni.Picha: DW/S. Wasilwa

Katika hotuba yake hiyo iliodumu kwa takriban dakika 37 huku ikiwa na wafuatiliaji zaidi ya elfu tano, Lisu ameishutumu serikali kwa madai kuwa imekuwa ikitumia njia mbalimbali katika kuua mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini humo ulioanza kufanya kazi kwa zaidi ya miongo miwili iliopita, huku mihimili ya bunge na mahakama ikitumika kushambulia mfumo huo wa demokrasia.

Aidha mwanasiasa huyo ametumia jukwaa hilo la kutangaza nia yake ya kuwania nafasi ya urais, kwa kuondoa sintofahamu ya sifa yake endapo ataruhusiwa kikatiba kuwania nafasi ya urais kutokana na yeye kuvuliwa nafasi ya uwakilishi wa wananchi katika bunge.

Tangazo lake lazusha mjadala Tanzania

Kutangaza nia kwa mwanansiasa huyo aliehudumu katika siasa kwa takriban miaka ishirini kumezua mjadala mpana katika jamii, huku wengi wakisema alipaswa kutolea hotuba yake akiwa hapa nyumbani na si ugenini, ili kujibu maswali ya wengi.

Juma lililopita chama kikuu cha upinzani nchini Chadema kilifungua mlango wake kwa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ambapo hadi sasa tayari wananachama wawili wameonesha wazi nia ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Mwandishi: Hawa Hawa Bihoga Dw Dar es salaam

Mhariri: Iddi Ssessanga