1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaanza awamu ya pili ya kuwasajili wapiga kura wapya

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi17 Januari 2022

Tume Huru ya kusimamia Uchaguzi nchini Kenya-IEBC, imeanza awamu ya pili ya kuwasajili wapiga kura kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/45cvd
Kenia | Präsidentschaftswahlen
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Tume hiyo iliyoshindwa kutimiza malengo ya kuandikisha wapiga kura milioni sita kwenye awamu ya kwanza iliyofanya mwaka uliopita inalenga kuandikisha wapiga kura milioni 4.5 wakati huu, zoezi hilo litakapokamilika tarehe sita Februari mwaka huu. 

Ili kufikia malengo yake kwenye zoezi hili, Tume ya IEBC imeambaza vifaa vya kuwasajili wapiga kura katika wadi zote kote nchini, huku ikilenga kuhakikisha kuwa wapiga kura milioni 25 wanashiriki katika upigaji kura, tarehe tisa Agosti mwaka huu. 

Tume hiyo ilianza zoezi la kuwaandikisha wapiga kura tarehe nne Oktoba hadi tarehe tano Novemba mwaka uliopita ambapo wapiga kura wapya milioni moja nukta tano waliandikishwa. Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema kuwa wataruhusu wapiga kura wanaotaka kubadilisha vituo vya upigaji kura ama nyaraka zao katika kipindi hiki.

Wapiga kura walioko nje ya nchi ya Kenya wataanza kuandikishwa tarehe 21 hadi tarehe sita mwezi Februari, zoezi hilo litakapokamilika. IEBC inalenga kuandikisha wapiga kura katika mataifa ya Uingereza, Marekani, Sudan Kusini, Quatar, Falme za Kiarabu na Ujerumani.

Awamu ya kwanza ya usajili ilishuhudia idadi ndogo ya watu waliojitokeza. Katika awamu ya pili, tume inalenga kuwasajili wapiga kura milioni 4.5
Awamu ya kwanza ya usajili ilishuhudia idadi ndogo ya watu waliojitokeza. Katika awamu ya pili, tume inalenga kuwasajili wapiga kura milioni 4.5Picha: Shisia Wasilwa/DW

Punde tu baada ya zoezi la kujiandikisha litakapokamilika, ukaguzi wa sajili ya wapiga kura itafanyika kisha walioandikishwa kudhibitishwa. Ukosefu wa vitambulisho kulisemekana kuchangia uandikishaji mdogo mwaka uliopita. Hata hivyo vijana wametoa sababu tofauti za kutojiandikisha kwa wingi.

Wakenya wanaoishi ughaibuni na wangependa kujisajili wameshauriwa kuwasilisha hati zao za usafiri na wawe na umri wa miaka 18 na zaidi kwa afisa wa usajili.

Hata hivyo Wakenya wanaioshi katika jumuiya ya Afrika Masharii watahitaji kutumia vitambulisho vyao kama ushahidi wa uraia wao kujisajili.

Uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2017, watu milioni 15.9 walisajiliwa kupiga kura.  Tume ya IEBC tayari imeidhinisha vyama 82 vya siasa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hata hivyo kinyang'anyiro kikuu kinatarajiwa kuwa kati ya makamu wa Rais William Ruto wa chama cha UDA na Raila Odinga ambaye amesema kuwa atawania kwa tiketi ya Muungano wa Azimio la Umoja.