1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya kulinda amani Congo yakabiliwa na kashfa za ngono

22 Septemba 2017

Shinikizo zazidi kutolewa kwa tume ya umoja wa mataifa ya kulinda amani kuwajibikia kesi za kashfa ya udhalilishaji wa kingono zinazoikumba tume yake nchini Congo.

https://p.dw.com/p/2kXgj
Demokratische Republik Kongo UN Friedenstruppe in Kinshasa
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompeng

Visa vingi vya udhalilishaji wa ngono vimeripotiwa nchini Congo. Yadaiwa maafisa wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakiwadhalilisha wanawake ikiwa ni pamoja na kuwabaka wanapokuwa wametumwa nchini humo.

Mmoja wa waathirika ni msichana mmoja wa miaka 14, yatima aliyenusurika vita na kukimbilia katika kambi ya umoja wa mataifa wa kulinda amani akidhani ni salama. Kumbe hakujua alikuwa anakimbia kufiwako na kuenda kuliwako nyama ambapo muathirika huyo anasema alishambuliwa na mmoja wa maofisa wa Umoja wa Mataifa raia wa Pakistani na kubakwa mbele ya ndugu zake.

Kisa hiki kilichoibua hisia kali na ambacho hadi leo kimesalia kuwa kitendawili licha ya juhudi zilizofanywa za kutafuta msaada, ni miongoni mwa vingine vingi ambavyo vinawaaibisha wanaolinda amani hadi umoja wa mataifa wenyewe.

Katika uchunguzi wa mwaka mmoja, shirika la habari la AP limebaini kuwa licha ya ahadi za mageuzi kwa zaidi ya muongo mmoja, umoja wa mataifa ulishindwa kufikia ahadi zake za kusitisha unyanyasaji huu au kutoa msaada kwa waathirika. Haki kwa waathirika ni kama ndoto kwani kesi zao hupotea au hupelekwa kwa nchi wanakotokea walindamani ambazo mara nyingi hazishughulikiwi. Umoja wa Mataifa umelaumiwa kwa kukandamiza juhudi za kuwatafutia haki waathirika hawa.

Imebainika kuwa kitovu cha visa vya unyanyasaji wa ngono vya Umoja wa Mataifa ni Congo ambapo upeo wa tatizo hili uliibuka miaka 13 iliyopita na marekebisho yalioahidiwa hayajafanyika. Kati ya malalamiko 2000 ya visa vya unyanyasaji yaliyofanywa dhidi ya umoja wa mataifa ulimwenguni zaidi ya miaka 12 iliyopita, shirika la habari la AP limegundua kuwa zaidi ya visa 700 vilitokea nchini Congo ambako ndiko kwenye tume kubwa ya amani ya Umoja wa Mataifa huku gharama kubwa za kulinda amani zikifikia dola billioni moja kila mwaka. AP iligundua pia waathirika wengi hawajapewa msaada huku wengi wanaopitia madhila pamoja na watoto wao wakitelekezwa na familia zao. Hadi leo ukatili huu bado unaendelea. Taifa la Congo pekee lina karibu thuluthi moja kati ya madai 43 yaliofanywa hadi mwaka wa 2017.

UN Soldat in Kongo Demokratische Republik Kongo
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akimsaidia mama na mwanawe kwenye msaada wa chakula nchini Congo.Picha: AP

Pia juhudi za mageuzi zinaathiriwa na kutokuweko kwa utaratibu wa kuhifadhi nyaraka kuhusu matukio yanayojiri. Umoja wa mataifa umekosolewa sana kwa hili na imebainika kuwa haijakuwa ikiweka rekodi ya matukio kabla ya mwaka wa 2010 kipindi ambacho madai yalikuwa yakiwekwa katika makundi mbali mbali, hatua inayolemaza msaada kwa waathirika.

Kulingana na Peter Gallo, mchunguzi wa zamani katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za uangalizi wa ndani amelaumu mfumo wa ukiritimba, na ulegevu kwa janga hili linaloendelea, ijapokuwa William Swing ambaye alikuwa akisimamia ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo kati ya mwezi Mei mwaka 2008 na Januari mwaka 2008, kipindi ambacho madai ya udhalilishaji yalipochacha, amekiri kubeba jukumu hilo na kusema kuwa makosa yaliyotokea miaka ya kwanza ya tume hiyo yatawapa mafunzo yatakayowasaidia katika kuleta mageuzi katika tume hiyo nchini Congo wakati ambapo ameteuliwa katika jopokazi la kukabiliana na tatizo hilo tena.

Hadi sasa Umoja wa mataifa unasema msaada hutolewa kwa wasichana wadogo na wanawake hata wakati wanaposubiri matokeo kujua baba za watoto lakini imeonekana hiyo ni kidogo sana, haswa kwa waathirika wanawake ambao walinyanyaswa kimapenzi nchini Congo kusalia na majukumu ya kulea watoto peke yao na wakiwa na umri mdogo.

Mwandishi: Fathiya Omar

Mhariri:Josephat Charo