1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Burundi yasema mauaji ya 1972 yalikuwa ya kimbari

21 Desemba 2021

Tume ya serikali ya Burundi iliyoundwa kuchunguza mauaji ambayo yameacha makovu katika nchi hiyo kwa mara ya kwanza imesema kuwa mauaji ya watu wengi wa kabila la Hutu nusu karne iliyopita yalikuwa mauaji ya halaiki. 

https://p.dw.com/p/44cRG
Burundi Gefängnis Feuer Brand Gitega
Picha: ASSOCIATED PRESS/AP/picture alliance

Tume hiyo ya Ukweli na Maridhiano – TRC iliundwa mnamo mwaka wa 2014 kuyachunguza maovu yaliyofanywa katika kipindi kibaya kabisa cha historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mivutano iliyotokota kwa muda ilisababisha vuguvugu la uasi wa Wahutu katika mwaka wa 1972 ambapo maelfu ya watu wa kabila la Tutsi waliuawa, na kisha baadaye kukatokea mashambulizi makali ya kulipiza kisasi ambayo wanaharakati wa Kihutu wanasema yalisababisha mauaji ya kati ya watu 100,000 na 300,000.

Mwenyekiti wa tume hiyo ya TRC  Pierre-Claver Ndayicariye ameliambia Bunge kuwa tume yake imeamua kuwa "uhalifu wa mauaji ya kimbari” ulifanyika dhidi ya Wahutu katika mwaka wa 1972 wakati wa serikali ya rais Michel Micombero, ambaye alikuwa wa kabila la Tutsi.

Mamia ya maelfu ya Warundi walikufa katika mawimbi ya machafuko ya kikabila na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu uhuru katika mwaka wa 1962, lakini umwagaji damu wa mwaka wa 1972 unazingatiwa kuwa mbaya kabisa.

Ndayicariye alisema jana katika hotuba yake ya saa tatu kuwa "uhalifu dhidi ya ubinaadamu” ulifanywa dhidi ya baadhi ya Watutsi katika kipindi hicho.

Mashuhuda waliiambia tume hiyo ya ukweli na maridhiano kuwa katika mwezi wa Mei na Juni mwaka wa 1972, Wahutu walisafirishwa kutoka jela katika eneo la Gitega kwenye malori kila usiku na kupelekwa kwenye kingo za mto Ruvubu, ambako waliuawa na kutupwa kwenye machimbo.

Ndayicariye amesema kuwa baada ya uchunguzi wa miaka mitatu, mabaki ya karibu watu 19,900 yalipatikana katika makaburi 200 ya halaiki. Tume hiyo imekabiliwa na tuhuma za kuyatumia vibaya mamlaka yake kwa kuangazia kazi ya kuchimbua katika maeneo ambayo Wahutu walizikwa na kuyapuuza yale walikozikwa wahanga wa Kitutsi.

Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Burundi inawajumuisha karibu makada wote wa chama tawala na Ndayicariye alikuwa mkuu wa tume ya uchaguzi ya Burundi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2010 na 2015.

AFP