1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras kusuka au kunyoa bungeni Athens

15 Julai 2015

Bunge la Ugiriki linapiga kura Jumatano kuamua juu ya masharti ya mageuzi yaliyotolewa na wakopeshaji ili nchi hiyo ipatiwe mkopo mkubwa wa uokozi, katika mtihani mgumu zaidi wa kisiasa kwa waziri mkuu Alexis Tsipras.

https://p.dw.com/p/1FygB
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.Picha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Waziri mkuu Tsipras alisema anabeba dhamana kamili kwa kusaini makubaliano ambayo hana imani nayo, lakini "niliyoyasaini kuepusha janga kwa uchumi wa nchi" iliyokuwa kwenye kingo za kuporomoka na kuondoka katika kanada ya sarafu ya pamoja. Katika makubaliano ya dakika za mwisho yaliyofikiwa siku ya Jumatatu, Tsipras alikubaliana juu ya mabadiliko makubwa ya sheria za kazi, malipo ya uzeeni, kodi ya ongezeko la thamani na kodi nyingine -- nyingi ya hizo zikiwa zilikataliwa na raia katika kura ya maoni ya umma -- ili Ugiriki ipatiwe fedha kunusuru uchumi wake usiporomoke.

Bunge mjini Athens laazima liidhinishe makubaliano kabla ya mataifa 18 wanachama wa kanda euro kuanza majadiliano juu ya kile Ugiriki itakachopata, ambao ni mkopo wa uokozi wenye thamani ya hadi euro bilioni 86, ambao utakuwa wa tatu katika kipindi cha miaka mitano. Lakini wakati muswada huo unatarajiwa kupita bungeni, Tsipras amelaazimika kuvigeukia vyama vya upinzani vinavyounga mkono Umoja wa Ulaya kuupitisha wakati ambapo anakabiliwa na upinzani kutoka wabunge 30 wa chama chake cha mrengo mkali wa kushoto Syriza, na kuibua maswali juu ya mustakabal wake wa kisiasa.

Bunge la Ugiriki linatrajiwa kuyapigia kura makubaliano ya uokozi Jumatano katika mtihani kwa waziri mkuu Tsipras.
Bunge la Ugiriki linatrajiwa kuyapigia kura makubaliano ya uokozi Jumatano katika mtihani kwa waziri mkuu Tsipras.Picha: Reuters

"Waziri mkuu laazima apambane, aseme ukweli, achukuwe maamuzi na asikimbie," Tsipras alisema katika mahojiano na televisheni ya Ugiriki alipoulizwa iwapo atajiuzulu ikiwa mageuzi hayo yatashindwa kupita bungeni, au akipoteza wingi wake bungeni. Matokeo ya uchunguzi wa maoni yaliyochapishwa Jumanne jioni na kituo cha utafiti cha Kapa yalibainisha kuwa asilimia 72 ya Wagiriki waliohojiwa walidhani makubaliano hayo yalikuwa muhimu, huku wengi wakiulaumu Umoja wa Ulaya kwa hatua kali, lakini wengi wanaiona kama fedheha kwa nchi ambayo bado inaendelea kuumizwa na miaka mingi ya kukaza mkwiji.

Mgomo wa watumishi wa umma

Watumishi wa umma wanatarajiwa kufanya mgomo wa masaa 24 Jumatano, wa kwanza mkubwa tangu Tsipras alipochukuwa madaraka, wakati wengi ndani ya chama cha Syriza wameapa kupiga kura ya hapana dhidi ya mipango hiyo, ambayo inakwenda kinyume na ajenda yao wenyewe. "Mashirika mengi zaidi ya Syriza yanapinga makubaliano haya.. kwa muktadha wa masuala ya ajira na pensheni huu ni mbaya kuliko mikopo miwili ya mwanzo," alisema naibu spika wa bunge Despoina Haralambidou katika mahojiano na kituo cha redio cha Vima FM.

Chini ya mpango mpya, kanda ya euro itachangia kati ya euro bilioni 40 na 50 kwenye mkopo mpya wa Ugiriki wa miaka mitatu, shirika la fedha la kimataifa IMF litachangia kiasi kingine kikubwa na fedha nyingine zitatokana na mauzo ya mali za serikali na masoko ya fedha, alisema afisa wa Umoja wa Ulaya. Mali za Ugiriki zilizopangwa kubinafsishwa zitawekwa kwenye mfuko maalumu wenye thamani ya hadi euro milioni 50, ambako kiasi cha euro bilioni 25 kati ya hizo zimepangiwa kuingizwa katika mfumo wa benki wa nchi hiyo.

Tsipras alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kunamaanisha akiba za Wagiriki wa kawaida ziko salama, lakini aliongeza kuwa kufunguliwa tena kwa benki -- ambazo zimefungwa kwa zaidi ya wiki sasa --kunategemea kukamilisha kwa makubaliano, ambayo yanaweza kuchukuwa mwezi. Benki kuu ya Ulaya imekuwa ikitoa fedha kwa benki za Ugiriki kuendelea kutoa huduma, lakini inaweza kulaazimika kukatisha msaada huo ikiwa Ugiriki itashindwa kufanya malipo makubwa inayotakiwa kuyafanya siku ya Jumatatu.

Katika kura ya maoni kuhusu mpango wa awali raia walisema "hapana". Je,bunge nalo litaukataa mpango mpya?
Katika kura ya maoni kuhusu mpango wa awali raia walisema "hapana". Je,bunge nalo litaukataa mpango mpya?Picha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Raia kuunga mkono

Tsipras amebashiri kuwa raia wengi zaidi wa Ugiriki wataunga mkono makubaliano, lakini anakiri kuwa "hawezi kusema kwa uhakika" kwamba yatatosha kuiepusha Ugiriki kuondoka katika kanda inayotumia sarafu ya euro ---kile kinachojulikana kama "Grexit" -- hadi makubaliano ya mwisho ya uokozi yasainiwe.

Akiongezea kwenye wasiwasi wake, afisa mwandamizi wa IMF alisema mfuko huo utashirki tu katika mpango wa tatu wa uokozi ikiwa wakopeshaji wake wa Umoja wa Ulaya watawasilisha mpango uliyo bayana wa usimamizi endelevu wa mkopo baada ya Ugiriki kushindwa kurejesha mikopo miwili katika kipindi cha wiki kadhaa. "Bila shaka makubaliano ya sasa siyo mapana na ya kina," alisema afisa huyo.

Shirika hilo la ukopeshaji lenye makao yake mjini Washington pia lilionya siku ya Jumanne kwamba wakopeshaji wa Ugiriki wa Umoja wa Ulaya watapaswa kwenda mbali zaidi ya makadirio yao ya sasa ya kusamehewa sehemu ya mkopo ili kutuliza sekta ya fedha ya nchi hiyo, akibainisha hatari kubwa za kifedha zinazohusiana na hasara.

Serikali za Umoja wa Ulaya pia zilipingana siku ya Jumanne kuhusiana na njia za kuisadia Ugiriki iweze kutimiza mahitaji yake ya kifedha wakati ikisubiri mkopo wa uokozi kukamilishwa, ambao unaweza kuchukuwa alau wiki nne. Wadai wa Ugirika wanakadiria kuwa nchi hiyo inahitaji euro bilioni 12 kuipeleka hadi katikati mwa mwezi Agosti -- zikiwemo euro bilioni 4.2 inazotakiwa kulipa kwa ECB siku ya Jumatatu -- lakini mataifa kama Uingereza yanapinga kuchangia kwenye ufadhili wowote wa muda.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekuwa nguzo muhimu katika harakati za kuinusur Ugiriki isifilisike.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekuwa nguzo muhimu katika harakati za kuinusur Ugiriki isifilisike.Picha: Reuters/E. Vidal

Jack Lew kuzuru Ujerumani, Ufaransa

Katika ishara ya wasiwasi unaoendelea kuhusiana na kutapaka kwa madhara yatokanayo na mgogoro wa Ugiriki, waziri wa fedha wa Marekani Jack Lew anatarajiwa kuzizuru Ujerumani na Ufaransa Jumatano na Alhamisi kwa ajili ya mazungumzo na mafisa wa ngazi za juu.

Ikiwa Ugiriki itafaulu kusaini makubaliano, hatua itakayofuata ya Ulaya ni kuidhinisha makubaliano hayo kupitia mabunge ya taifa, mengi yao katika mataifa yasiyotaka kuipa Ugiriki msaada zaidi. Bunge la Ujerumani linatazamiwa kupigakura siku ya Ijumaa, ikiwa bunge la Ugiriki litaharakisha kupitisha sheria mpya kufikia mwisho wa Jumatano hii.

Uchunguzi mpya wa maoni ulisema asilimia 55 ya Wajerumani wanamuunga mkono Kansela Angela Merkel kuhusu makubaliano ya uokozi, wakati theluthi moja wangependelea "Grexit." Tsipras alisema ataitetea serikali yake dhidi ya "mipango ya baadhi wahafidhina wa Ulaya" na kukosoa "Plan B" ya kuondoka kwa taifa lake kutoka euro, uliyopendekezwa na waziri wa fedha wa Ujerumani. "Ulaya siyo ya (Wolfgang) Schaeuble," alisema.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman