Tshisekedi awataka waasi Kongo kuweka chini silaha
15 Agosti 2023Ametoa wito huo katika siku ya pili ya mkutano wa kutathmini hali ya dharura iliyotangazwa katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini miaka miwili iliyopita. Mashirika ya kiraia yanasema utawala wa kijeshi uliowekwa katika mikoa hiyo chini ya hali hiyo ya dharura umeshindwa kurejesha amani na usalama, na kutaka ukomeshwe.
Mkutano huo ulioitishwa na serikali ya Kongo unawakutanisha hapa Kinshasa tangu jana Jumatatu, baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kijamii pamoja na wale wa mashirika ya kiraia ili kutathmini kwa usahihi, hali ya mzingiro yaani utawala wa kijeshi huko Ituri na Kivu Kaskazini. Rais Félix Tshisekedi aliwataka washiriki kuchukua hatua zozote zinazohitajika ili kurejesha amani na usalama katika mikoa hiyo miwili. Alitoa wito kwa waasi na makundi mengine yanayomiliki silaha kuchukua fursa ya mwisho iliyotolewa na serikali kwa ajili ya amani.
"Siwezi kumaliza hotuba yangu bila kutoa wito wa kizalendo kwa Wakongo ambao kwa bahati mbaya bado wanafanya vitendo vya uasi dhidi ya nchi hii. Napenda kulihakikishia taifa kuwa serikali imejitolea kwa nia njema kutoa fursa ya mwisho kwa makundi ya uasi kujisalimisha kwa amani."
Mikoa ya Ituri na Kivu kaskazini imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu Mei 6 mwaka 2021. Utawala maalum ulioamriwa na Rais Tshisekedi kwa lengo la kurejesha amani na mamlaka ya Serikali huko. Lakini wakazi wa mikoa hiyo miwili wanatarajia tu mkutano wa Kinshasa kukomesha hali hiyo ya kuzingirwa, kama alivyoeleza Dieudonné Lossa Dekhana, mratibu wa mashirika ya kiraia mkoani Ituri.
"Hakuna hata kundi linalomiliki silaha lililoondolewa katika eneo la Ituri. Idadi ya makundi yenye silaha imeongezeka wakati wa hali ya kuzingirwa na tumeorodhesha watu kadhaa waliouawa na wengine kadhaa kuyahama makazi yao. Wakazi wa Ituri wanatarajia tu kukomeshwa hali ya kuzingirwa kwani haikukuwa na ufanisi."
Wahudhuriaji mkutano huo wana siku tatu za kujadili na kutoa mapendekezo. Yaani kazi ya mkutano huo inaendelea hadi kesho Jumatano