Tshisekedi ajiapisha Rais!
24 Desemba 2011
Tshisekedi alieshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi wa Novemba aliipinga amri ya polisi ya kumkataza kujiapisha kuwa Rais, hatua aliyoipanga kuitekeleza kwenye uwanja wa kandanda katika mji Mkuu, Kinshasa.
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuzizuia sherehe alizozipanga kuzifanya kiongozi huyo wa upinzani ambae sasa ana umri wa miaka 79. Kutokana na magari ya deraya ya jeshi la ulinzi na idadi kubwa ya polisi waliokusanywa kwenye uwanja wa kandanda, Tshisekedi alizihamishia sherehe za kujiapisha nyumbani kwake. Lakini huko pia polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwashambulia wafuasi na viongozi wa chama cha Tshisekedi cha Umoja wa Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii waliokusanyika nje ya nyumba yake.
Duru iliyo karibu na Mkuu wa Polisi ya nchi ,imesema kuwa tayari yupo Rais aliechaguliwa na aliekwishaapishwa. Kwa mujibu wa duru hiyo Polisi imesema kuwa haiwezekani kufanyika sherehe nyingine za kuapishwa kwa Rais.
Polisi imesema sherehe hizo ni kitendo cha uchochezi. Tshisekedi alikula kiapo cha Biblia baada ya mkuu wake wa utumishi, Albert Moleka kusoma tamko kudai kwamba hatua isiyofutika imechukuliwa katika historia ya nchi iliyotoka kwenye udikteta wa Rais Kabila na wafuasi wake na kuingia katika demokrasia halisi.
Msemaji wa serikali Lambert Mende haraka sana alizipuuza sherehe za kuapishwa Tshisekedi kuwa udanganyifu na kashfa! Bwana Mende amesema , Mkuu wa nchi anaapishwa mbele ya Mahakama Kuu. Aliuliza iwapo watu walimwona Jaji Mkuu kwenye kiapo cha Tshisekedi? Rais Kabila aliapishwa rasmi jumanne iliyopita kwenye sherehe zilizofanyika mjini Kinshasha. Mpinzani wake Mkuu Tshisekedi anadai kwamba alinyang'anywa ushindi kutokana na wizi mkubwa wa kura.
Katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita, Rais Kabila alipata asilimia karibu 49 wakati Tshisekedi alipata asilimia 32.
Mwandishi/Habibou Hangre/AFPE/
Tafsiri/Mtullya Abdu/