1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Tsai:Mazoezi ya jeshi la China yaondoa utulivu wa kikanda

11 Aprili 2023

Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen amesema mazoezi ya kijeshi ya China kukizunguuka kisiwa hicho yamesababisha kukosekana utulivu kwenye ukanda mzima na kukitaja kitendo hicho ni kutowajibika kwa taifa kubwa kama China.

https://p.dw.com/p/4Pt2H
Taiwans Präsidentin Tsai Ing-wen
Picha: Taiwan Presidential Office/AP/picture alliance

Kupitia ukurasa wake wa Facebook rais Tsai ameandika, kama rais anawakilisha taifa lake duniani na ziara zake nje ya nchi ikiwemo Marekani si jambo geni na kuongeza kwamba China ilitumia mwanya huo kuanzisha mazoezi ya kijeshi hatua ilioondoa utulivu kwa Taiwan na kanda kwa ujumla wake.

Matamshi hayo ameyatoa wakati China tayari imemaliza mazoezi yake ya kijeshi ya siku tatu yaliopewa jina la "upanga wa Pamoja" ikiyataja yenye mafanikio makubwa.

Soma pia:China yahitimisha luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan

Hapo awali wizara ya Ulinzi ya kisiwa hicho ilisema ilibaini kuwepo kwa meli 12 za kivita za China pamoja na ndege 91 siku ya Jumatatu.

Wizara hiyo ilisema ndege ya kivita chapa J15 iliruka kutoka meli ya Shandong na ilikuwa mojawapo kati ya ndege 54 zilizovuuka mpaka na kuingia anga ya Taiwan.

China na mshirika wake Urusi watetea luteka hizo

Taarifa iliyotolewa na Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la Ukombizi wa Watu, PLA, ilisema "mazoezi hayo yalijaribu kwa kina uwezo wa pamoja wa matawi ya kijeshi kushambulia kwenye mazingira halisi."

Chinas dreitägige Militärübungen rund um Taiwan
Wachina wakiangalia mazoezi ya kijeshi kuzunguuka Tawaina Picha: Tingshu Wang/REUTERS

Taarifa hiyo iliongeza kwamba wanajeshi wa China walikuwa "tayari kwa mapambano na wanaweza kupigana wakati wowote, na watakabili kwa nguvu zote "namna yoyote ya hisia za kujitenga kwa Taiwan na majaribio ya uingiliaji kati wa kigeni."

Soma pia:Taiwan yabain ndege za kivita 59 na meli 11 za China

Mshirika wa karibu wa China, Urusi, ilitetea mazoezi hayo ya kijeshi, huku msemaji wa Ikulu ya Kremlin alisema "Beijing ina haki ya kulinda mamlaka yake na kujibu matendo ya uchokozi."

China ambayoiliionya Marekani kumruhusu Tsai kukutana na Spika wa Bunge Kelvin McCarthy haijasita kufikiria kutumia nguvu kukirudisha Kisiwa hicho kinachojitawala kidemocrasia chini ya udhibiti wa Beijing.