Trump aziwashia moto nchi za NATO
12 Julai 2018Rais Donald Trump wa Marekani ameendeleza kauli kali dhidi ya washirika wanaounda jumuiya ya Kujihami ya NATO, akisema marais wengi wa Marekani walikuwa wakijaribu bila mafanikio kwa miaka mingi kuilazimisha Ujerumani na nchi nyingine tajiri za NATO kuongeza bajeti za ulinzi dhidi ya Urusi na hivyo kuiacha Marekani pekee ikilipa mabilioni ya dola kwa ajili ya ulinzi.
Rais Trump anazitaka nchi tajiri zilizoko katika Jumuiya hiyo ya NATO na hasa Ujerumani, Ubelgiji na Uhispania zitenge asilimia 4 ya pato jumla la nchi zao katika bajeti ya ulinzi, akidai kwamba Marekani inatumia mabilioni ya dola kuiruzuku Ulaya. Trump amechukua msimamo wa kibabe katika mkutano huo wa kilele wa NATO akihoji thamani ya muungano huo ambao umekuwa ukiielekeza sera ya nje ya Marekani kwa miongo kadhaa na kuwamulika washirika wa nchi yake pamoja na kupendekeza ongezeko kubwa la matumizi ya kijeshi katika nchi za Ulaya.
Trump pia alikabiliwa vilivyo na nchi za Ulaya kwa kumkumbatia Rais Vladmir Putin wa Urusi lakini akaigeuzia kibao Ujerumani akimulika uhusiano wa nchi hiyo ya Urusi na kudai kwamba serikali ya Kansela Angela Merkel imejiachia na kudhibitiwa kikamilifu na kutekwa nyara na Urusi kutokana na maslahi ya kutaka bomba la gesi asilia kutoka Urusi. Amedai Ujerumani imeanza kuiilipa Urusi mabilioni ya fedha kwa ajili ya mahitaji yao ya nishati kutoka bomba la Urusi, na hilo ni jambo lisilokubalika. Lakini kabla ya kikao cha leo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliwaambia waandishi habari kwamba kila kitu kitakwenda shwari katika kikao hicho.
Wakosoaji wanahisi msururu wa kauli mpya za Trump na hasa za kulazimisha nchi wa Ulaya ziongeze kiwango cha bajeti ya ulinzi zinatishia kuhujumu muungano huo wa miongo kadhaa ulioanzishwa kwa lengo la kukabiliana na uchokozi wa uliokuwa Muungano wa Sovieti.
Kansela Merkel ambaye binafsi alilelewea katika Ujerumani Mashariki ya kikomunisti amezungumzia jinsi alivyowahi kushuhudia hali ya kudhibitiwa na muungano wa Usovieti na kwamba anafurahi wakati huu kwamba kuna mshikamano katika uhuru kama Jamhuri ya shirikisho la Ujerumani. Amesisitiza juu ya mshikamano wa Jumuiya ya NATO katika kuamua sera zao. Bi Merkel amesema si kweli kuwa nchi yake imechukuliwa mateka na Urusi kama anavyodai Rais Trump.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May pia ametowa mwito wa mshikamano miongoni mwa washirika wa NATO, akitaja kwamba wakati Urusi inashirikishwa lazima suala hilo lifanyike chini ya msimamo mmoja wa mshikamano na udhabiti katika NATO. Baada ya Brussels, Trump atakwenda Uingereza ambako serikali ya May iko katika mkwamo mkubwa kuhusiana na mipango ya kujitowa Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/Reuters/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Khelef