Trump ayataka mataifa ya Ulaya kuwapokea IS kutoka Syria
17 Februari 2019"Marekani inazitaka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na mataifa mengine washirika wa Ulaya kuwachukua zaidi ya wapiganaji 800 ambao wamekamatwa nchini Syria na kuwafikisha mahakamani," rais huyo aliandoka katika mfululizo wa maandishi yake katika ukurasa wa Twitter. "Eneo la Ukhalifa linakaribia kuanguka. Mbadala wake sio mzuri kwa sababu tutalazimika kuwaachia huru.
"Marekani haitaki kuwa walinzi wa wapiganaji hawa wa ISIS kutoka Ulaya, ambako ndiko wanatarajiwa kwenda.
"Tunafanya mengi na tunatumia fedha nyingi, sasa wakati umefika kwa wengine kuchukua jukumu hilo na kufanya kazi ambao wanaweza sana kuifanya. Tunaondoa majeshi yetu baada ya ushindi wa asilimia 100 dhidi ya sehemu hiyo ya Ukhalifa!"
Maandishi yake katika Twitter yanakuja baada ya makamu wa rais Mike Pence kutoa wito kwa mataifa mengine kuchukua jukumu nchini Syria wakati vikosi vya jeshi la Marekani vikiondolewa.
Pembezoni mwa mkutano wa usalama mjini Munich, aliwaambia waandishi habari kwamba Marekani inataka mataifa mengine kutoa vikosi vya jeshi na mengine vifaa kusaidia kuilinda Syria.
Trump azusha wasi wasi
"Tunayaomba mataifa mengine kujiunga nasi na kutupatia vifaa na msaada na vikosi vitakavyowezesha kulinda maeneo na kuwazuwia wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu ama kundi lolote la itikadi kali kuweza kuzuka na kuchukua tena maeneo yaliyokombolewa," amesema.
Trump alisababisha wasi wasi mkubwa mwezi Desemba wakati ghalfa alipotangaza kwamba Marekani itaondoa majeshi yake kutoka Syria na kwamba kundi linalojiita Dola la Kiislamu tayari limeshindwa.
Wakosoaji walionya kwamba kundi hilo la kigaidi halijashindwa na kumalizwa na kwamba kujiondoa kwa Marekani kunaweza kusababisha kufufuka kwa kundi hilo, ambapo washirika wa Marekani katika eneo hilo hawana uwezo wa kupambana na kitisho hicho peke yao.
Majeshi ya kundi la Syrian Democratic Forces SDF , kundi la wanamgambo wanaoongozwa na Wakurdi wakiungwa mkono na Marekani walianzisha mashambulizi wiki iliyopita kuwaondoa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu katika kijiji cha Baghuz, eneo pekee lililoko chini ya udhibiti wao, karibu na mpaka na Iraq.
Pia kuna hofu kwamba bila ya kuwapo majeshi ya Marekani, Uturuki inaweza kufanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa SDF, ambao wengi wao ni wapiganaji wa vikundi vya ulinzi wa umma vya jamii ya Wakurdi yaani YPG.
Uturuki inawaona wapiganaji hao wa YPG kuwa ni kundi linalotokana na kundi linalotaka kujitenga nchini Uturuki la Workers' Party PKK, ambalo limepigana vita vya miongo kadhaa upande wa kusini mwa nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Zainab Aziz