1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aweka vitisho zaidi vya ushuru kwa China

6 Aprili 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amewaagiza maafisa wa biashara wa nchi hiyo kufikiria kuongeza ushuru mwingine wa Dola bilioni 100 kwenye bidhaa za China zinazoingia Marekani.

https://p.dw.com/p/2vaXF
Symbolbild zur drohenden Zuspitzung des Handelskrieg s zwischen den Vereinigten Staaten von Amerika
Picha: imago/R. Peters

Trump ametoa maagizo hayo siku chache baada ya kutangaza kuzitoza ushuru bidhaa za China zenye thamani ya Dola bilioni 50. Hatua hiyo inazidi kuongeza mzozo wa kibiashara ulioko kati ya China na Marekani. Trump amefikia uamuzi huo jana, baada ya China kutangaza orodha ya bidhaa muhimu za Marekani ambazo pia ushuru wake utaongezeka, ikiwemo maharage ya soya pamoja na ndege ndogo, iwapo Marekani itaanza kutoza ushuru mpya iliyotangaza awali.

Trump amefafanua kuwa kutokana na China kujihusisha tena katika biashara isiyozingatia haki, ameliagiza baraza la biashara la Marekani, USTR kufikiria kama nyongeza ya ushuru wa bidhaa zenye thamani ya Dola bilioni 100 utakuwa sahihi.

Amesema maafisa wa biashara wa Marekani wamebaini kuwa uchunguzi wa kipengele cha 301 ambacho kinatoa idhini ya matumizi ya ushuru dhidi ya China, umeonyesha kwamba serikali ya China imekuwa ikitumia vibaya ujuzi na haki miliki za Marekani kupitia mahitaji ya mradi wa pamoja ambao mara nyingi hauwezi kujadiliwa bila kuhamisha teknolojia. Hata hivyo China imekanusha madai hayo.

China US-Produkte im Supermarkt
Mwananchi wa China akinunua bidhaa kutoka Marekani Picha: picture alliance/AP Photo/Andy Wong

Saa chache baada ya Trump kutoa tangazo hilo, China imemjibu kiongozi huyo ikiapa kupambana na Marekani kwa gharama yoyote ile katika vita ya kibiashara na itahakikisha inayalinda maslahi yake. Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China, Lu Kang amesema nchi yake haina mpango wa kuingia katika vita vya kibiashara, lakini haiogopi kupambana na yeyote yule na kwamba mzozo wa kibiashara umeanzishwa na Marekani.

''Kama Marekani itaendelea kuipuuza China na jumuiya ya kimataifa na kusisitiza kuhusu kulinda biashara zake, basi China itapambana hadi mwisho. China itaendelea kuimarisha mageuzi yake, kufungua na kuulinda mfumo wa biashara ya kimataifa pamoja na kukuza uhuru wa biashara na uwekezaji,'' alisema Kang.

Tayari China imefungua madai katika Shirika la Biashara Duniani, WTO, kupinga ushuru wa awamu ya kwanza uliotangazwa na Trump. Kiongozi huyo wa Marekani amesema ataweka ushuru katika bidhaa za chuma na aluminium ambazo zitaingizwa nchini mwake kutoka China.

Kwa upande wake China ililipiza kisasi kwa kuweka ushuru kwenye bidhaa za Marekani zinazoingia nchini humo ikiwemo matunda, nguruwe na aluminium kwa ajili ya matumizi mapya, zote zikiwa na thamani ya Dola bilioni tatu.

Lakini inaonekana kuwa Trump yuko tayari kwa mazungumzo iwapo China itataka kufanya hivyo. Utafiti uliofanywa wiki iliyopita na taasisi ya Brookings yenye makao yake mjini Washington, umeonyesha kuwa kiasi ya ajira milioni 2.1 za Marekani huenda zikaathiriwa na mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga