Trump awasili China
8 Novemba 2017Trump amewasili leo kwenye mji mkuu wa China, Beijing akiwa na mkewe Melania na kupokelewa kwa bendi ya jeshi kabla ya kuelekea Forbidden City ambako kuna makumbusho ya kasri la kifalme, mji ambao anakutana na Rais Xi pamoja na mkewe Peng Liyuan.
Saa chache kabla ya kuwasili mjini Beijing, Trump aliitolea wito China kusaidia katika kukabiliana na uchokozi unaofanywa na Korea Kaskazini kutokana na mpango wake wa nyuklia. Ikulu ya Marekani imesema Trump ataitumia ziara hiyo kuiomba China kusitisha uhusiano wake wa kifedha na Korea Kaskazini na kuheshimu vikwazo vya Umoja wa Mataifa. China ni mshirika mkubwa wa kibiashara na Korea Kaskazini.
Akiwa Korea Kusini kiongozi huyo wa Marekani alizitaka China na Urusi kusaidia kuiwekea shinikizo Korea Kaskazini kusitisha kutengeneza silaha za nyuklia na kuileta nchi hiyo katika meza ya mazungumzo. Akizungumza katika Bunge la Korea Kusini mjini Seoul, Trump ametoa onyo kali kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ambapo amemtaka asiwadharau na wala asiwajaribu.
''Hatuwezi kuruhusu Marekani au washirika wetu kushambuliwa. Hatuwezi kuruhusu miji ya Marekani itishiwe na silaha za maangamizi. Hatutoogopa. Na hatutoruhusu ukatili mwingine ujirudie katika historia, kwenye ardhi hii ambayo tuliipigania na kufa kwa ajili ya kuilinda,'' alisema Trump.
Rais Trump amezitaka Urusi na China kusitisha uhusiano wowote na Korea Kaskazini, ukiwemo ule wa kidiplomasia. Aidha, amesema muda wa kutoa sababu na visingizio umekwisha na kwamba sasa ni wakati wa kuwa imara, kwani mtu anayetaka amani lazima asimame imara wakati wote.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesisitiza kwamba nchi hiyo imewahi kutekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Korea Kaskazini, lakini imesema itachunguza iwapo kuna shughuli ambazo zinakiuka maazimio hayo. Kwa mujibu wa wizara hiyo, China bado ina matumaini ya kuutatua mzozo uliopo kwa njia ya mazungumzo.
Kwa upande wa masuala ya kibiashara, Trump bado yuko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashirika ya biashara ya Marekani katika kutatua malalamiko ya kibiashara na China. Marekani imeishutumu China kwa kurudia ahadi yake ya kufungua masoko yake. Wiki iliyopita Trump alisema kulikuwa na hasara ya kibiashara ya Dola bilioni 347 kati ya nchi hiyo na China na kwamba hatua hiyo ni mbaya na inatia aibu.
China ni kituo cha tatu cha ziara ya siku 12 ya Trump barani Asia ambayo itamfikisha pia Vietnam na Ufilipino. Tayari kiongozi huyo wa Marekani ameizuru Japan na Korea Kusini.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, http://bit.ly/2iDsZsU
Mhariri: Josephat Charo